Michezo

Kenya kuwa mwenyeji wa marudiano ya mechi ya AFCON kati ya Uganda na Sudan Kusini

October 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KENYA itakuwa mwenyeji wa mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 itakayowakutanisha Uganda na Sudan uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Novemba 17, 2020.

Vikosi hivyo vitakutana kwanza jijini Kampala, Uganda mnamo Novemba 9 kabla ya kurudiana jijini Nairobi siku nane baadaye.

Sudan Kusini kwa sasa hawana uwezo wa kuandaa mechi yoyote ya kimataifa kwa sababu uwanja wa Kitaifa wa Juba unafanyowa ukarabati.

Shughuli za kukarabatiwa kwa uwanja huo ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 7,000 walioketi zilianza Aprili 5, 2019 na zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa 2020. Ukarabati huo unaodhaminiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), unatarajiwa kugharimu kima cha Sh500 milioni.

Uganda kwa sasa wanaongoza Kundi B kwa alama nne kutokana na mechi mbili. Burkina Faso na Malawi wanashikilia nafasi za pili na tatu mtaliwa huku Sudan Kusini wakivuta mkia baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Malawi ugenini kabla ya kupigwa 2-1 na Burkina Faso jijini Khartoum mnamo Novemba 2019.

Uganda na Sudan Kusini watakaposhuka dimbani, macho ya mashabiki wa soka ya humu nchini yataelekezwa zaidi kwa sajili mpya wa Gor Mahia, Tito Okello. Katika mahojiano yake na Taifa Leo hivi majuzi, Okello alikiri kwamba ilimchukua zaidi ya miaka mitatu kuamua iwapo atachezea Uganda au Sudan Kusini.

Hadi alipoingia katika sajili rasmi ya Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi na washindi mara 19 wa KPL, Okello aliwahi pia kuchezea BUL, African Lyon, Benfica De Macau, KCCA na mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Uganda, Vipers SC.

Okello alisema aliteua kuchezea timu ya taifa ya Sudan Kusini kwa sababu walimthamini na kuridhishwa zaidi na ukubwa wa uwezo wake tangu zamani.

“Sudan Kusini wana imani kubwa kwangu. Walianza kunimezea tangu zamani na wakawa radhi kunipa uraia ili niwachezee katika kiwango cha timu ya taifa,” akasema Okello.