Michezo

Kenya Lionesses waanza Krakow Challenger Series kwa kurarua Ubelgiji

Na GEOFFREY ANENE April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA Lionesses wameanza vyema duru ya mwisho ya msimu wa kawaida ya raga za saba kila upande za Challenger Series baada ya kurarua Ubelgiji 12-0 mjini Krakow nchini Poland mnamo Ijumaa, Aprili 11, 2025.

Sinaida Nyachio alifungia Kenya alama zake zote katika mechi hiyo ya Kundi A.

Nyachio alitinga mguso wa kwanza chini ya milingoti sekunde ya mwisho ya kipindi cha kwanza baada ya kuwamwaga walinzi wa Ubelgiji kwa kudanganya anapasiana mpira ndani ya kisanduku cha mita 22 na kufyatuka hadi kinsaduku cha miguso.

Aliongeza mkwaju wa mguso huo na kuweka Kenya kifua mbele 7-0 wakati wa mapumziko.

Vipusa wa kocha Dennis Mwanja waliona lango tena kupitia Nyachio sekunde ya mwisho ya kipindi cha pili, mara hii akitinga kwa kona.

Wakenya, ambao walishinda duru mbili za kwanza mjini Cape Town nchini Afrika Kusini mwezi Machi, wako nafasi ya pili kundini mwao nyuma ya Thailand.

Thailand walilemea Colombia 24-12 katika mechi ya ufunguzi.

Kenya itakabana koo na Thailand (3.20pm) na kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Colombia (6.28pm).

Timu nne-bora kutoka ligi hiyo ya mataifa 12 baada ya duru zote tatu kujumlishwa wataingia mashindano ya muondoano mjini Los Angeles nchini Amerika mwezi ujao kupepetana na nne za mwisho kutoka Raga za Dunia 2024-2025 (Brazil, Uchina, Ireland na Uhispania) kutafuta tiketi nne za kushiriki Raga za Dunia 2025-2026.

Duru ya Krakow inahusisha timu nane-bora baada ya duru mbili za kwanza.

Uganda, Hong Kong, Samoa na Mexico walibanduliwa baada ya kumaliza duru mbili za kwanza nje ya nane-bora.

Kundi B linajumuisha Argentina, Afrika Kusini, Czech na Poland.