Kenya Lionesses yaanza kampeni ya kuingia Kombe la Dunia kwa kurarua Madagascar
Na GEOFFREY ANENE
KENYA imetoka chini alama tano na kulipua Madagascar 35-5 Ijumaa katika mechi yake ya ufunguzi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande ya wanawake mjini Brakpan, Johannesburg nchini Afrika Kusini, Ijumaa.
Warembo wa kocha Felix Oloo walisawazisha 5-5 kupitia mguso wa Celestine Masinde dakika ya 20 baada ya wanavisiwa wa Madagascar kutangulia kuona lango dakika mbili mapema kupitia kwa Patricia Ravololonirina.
Janet Okelo aliweka Kenya mbele 10-5 dakika ya 35 kabla ya nahodha Philadelphia Olando kupachika mguso dakika tano baadaye ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Irene Atieno, huku Kenya ikifurahia uongozi wa 17-5 wakati wa mapumziko.
Kenya ilianza kipindi cha pili kwa kufunga mguso bila mkwaju kutoka kwa Diana Awino dakika ya 55 kabla ya kupata pigo Atieno alipolishwa kadi ya njano dakika tatu baadaye kwa kucheza visivyo na kukalishwa nje.
Hata hivyo, ikiwa na wachezaji 14 uwanjani baada ya Mercy Migongo kuonyeshwa kadi ya njano, Kenya ilizidi kutafuta alama zaidi na kuimarisha uongozi wake wa 27-5 kupitia kwa Christabel Lindo dakika ya 67.
Nahodha msaidizi Janet Owino aliandikisha jina lake katika orodha ya wafungaji kupitia penalti dakika ya 74 na kuiweka mbele 30-5.
Masinde alipata mguso wake wa pili wa mechi alipopachika mguso sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kulia.
Kenya itakutana na Lady Cranes ya Uganda katika mechi yake ijayo mnamo Agosti 13 na kukamilisha mashindano haya ya mataifa manne dhidi ya miamba Afrika Kusini mnamo Agosti 17.
Mshindi wa mashindano haya ataingia moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia nchini New Zealand mwaka 2021.
Afrika Kusini, ambayo ndiyo timu pekee imewahi kuwakilisha Bara Afrika katika Kombe la Dunia la wanawake iliposhiriki makala ya mwaka 206, 2010 na 2014, imeratibiwa kufungua kampeni yake dhidi ya Uganda baadaye Ijumaa.