Kenya Simbas yashuka viwango bora vya raga duniani
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Kenya almaarufu Simbas imeteremka kutoka nafasi moja hadi nambari 34 katika viwango bora vya Shirikisho la Raga Duniani (World Rugby) vilivyotangazwa Jumatatu.
Simbas pamoja na Zimbabwe, ambazo zitakutana katika mechi ya mwisho ya shindano la mataifa manne la Victoria Cup mnamo Septemba 21 jijini Nairobi, zimerukwa na Colombia iliyotitiga Paraguay 54-15 (Agosti 28) na Mexico 51-24 (Agosti 31) katika mashindano ya Bara America almaarufu Americas.
Colombia inashikilia nafasi ya 32 baada ya kuruka juu nafasi mbili ikifuatiwa na Zimbabwe na Kenya katika usanjari huo.
Afrika Kusini na Namibia zinashikilia nafasi mbili za kwanza barani Afrika katika nafasi ya tano na 23 duniani, mtawalia. Zimbabwe na Kenya zinafuatana katika nafasi ya tatu na nne barani Afrika.
Uganda imerukia nafasi ya tano barani Afrika na 41 duniani baada ya kupepeta Zambia 35-28 katika mechi ya Victoria Cup jijini Lusaka, wikendi.
Ufilipino na Ivory Coast zimeshuka nafasi moja hadi nambari 42 na 43 duniani baada ya Uganda kuimarika. Ivory Coast ni ya sita barani Afrika. Inafuatiwa na Morocco, ambayo imeteremka duniani kutoka 47 hadi nambari 48 nazo Madagascar na Senegal zimepaa nafasi moja hadi nambari 52 na 54 duniani, mtawalia. Zambia inasalia katika nafasi ya 65 duniani katika viwango hivi vya mataifa 105.
New Zealand imerejea katika nafasi ya kwanza duniani kutoka nafasi ya pili baada ya kunufaika na Wales kuchapwa 22-17 na Ireland katika mechi ya kupimana nguvu kabla ya Kombe la Dunia. Baada ya ushindi huu, Ireland pia imeimarika kutoka nafasi ya nne hadi nambari mbili nayo Uingereza inasalia katika nafasi ya tatu. Wales imerushwa hadi nafasi ya nne.