• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Kenya tayari kwa kivumbi cha raga ya makinda U-20

Kenya tayari kwa kivumbi cha raga ya makinda U-20

Na MWANDISHI WETU

TIMU za taifa za Namibia, Tunisia na Senegal zinatua leo Jumanne jijini Nairobi kwa mashindano ya raga ya Bara Afrika ya wachezaji 15 kila upande kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 almaarufu Barthes Cup yatakayofanyika Aprili 4-7 katika klabu ya michezo ya KCB mtaani Ruaraka.

Senegal itakuwa ya kwanza kuwasili muda wa saa kumi na moja asubuhi ikifuatiwa na Tunisia saa mbili asubuhi nayo Namibia imeratibiwa kuingia Kenya saa tisa alasiri.

Mashindano ya Barthes Cup yatajumuisha timu nne (Kenya, Namibia, Tunisia na Senegal).

Mabingwa watetezi Namibia watalimana na Senegal katika nusu-fainali ya kwanza saa saba unusu Aprili 4 kabla ya Chipu ya Kenya kuvaana na Tunisia katika nusu-fainali ya pili saa mbili baadaye.

Washindi wataingia fainali kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki mashindano ya dunia ya World Junior Rugby Trophy (JWRT).

Timu zitakazopoteza katika nusu-fainali zitashindania nafasi ya tatu.

Mshindi wa medali ya shaba atasalia katika ligi hii ya juu kwa mwaka mwingine naye atakayepoteza mchuano huu atatemwa hadi daraja ya pili.

Kocha Paul Odera alitarajiwa kutangaza kikosi chake cha Kenya cha wachezaji 25 jana baada ya kuandaa kambi ya siku mbili uwanjani RFUEA Grounds.

Kiingilio uwanjani Ruaraka ni Sh300 kila siku.

Kenya iliwahi kushiriki mashindano ya JWRT baada ya kuwa mwenyeji uwanjani RFUEA mwaka 2009. Kwingineko, timu za taifa za raga za Kenya za wachezaji saba kila upande za Shujaa (wanaume) na Lionesses (wanawake) zilitarajiwa Jumatatu usiku kuwasili Hong Kong.

Lionesses ya kocha Kevin Wambua iliondoka nchini Machi 31 saa tano usiku kuelekea Hong Kong kwa mchujo wa kutafuta tiketi ya kushiriki Raga ya Dunia ya Wanawake msimu 2019-2020 utakaofanyika Aprili 4-5.

Mabingwa hawa wa Afrika watakabiliana na Papua New Guinea, mahasimu wa tangu jadi Uganda na wenyeji Hong Kong katika mechi za kundi B.

Shujaa ya kocha Paul Murunga inashiriki Raga ya Dunia ya wanaume.

Itamenyana na Fiji, New Zealand na Australia katika duru ya Hong Kong itakayofanyika Aprili 5-7. Vijana wa Murunga wanashikilia nafasi mbaya kwenye jedwali ya 14 ambapo wako katika ulazima wa kujitahidi zaidi kuingia robo-fainali kuu kutoka kundi hili la kifo.

Wamezoa alama 18, nne zaidi ya nambari 15 Japan, ambayo inashikilia nafasi ya kutemwa kutoka ligi hii ya nchi 15.

Kenya ilipigwa jeki na kurejea kikosini kwa wachezaji sita wazoefu baada ya kugoma tangu msimu uanze Desemba mwaka jana. Wachezaji hao ni Andrew Amonde, Augustine Lugonzo, Nelson Oyoo, Eden Agero, Daniel Sikuta, Jeffrey Oluoch na Oscar Dennis.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa kando hukasirika nikimpigia...

Real Madrid kuamua hatima ya Bale mwishoni mwa msimu

adminleo