Michezo

Kenya U-17 yacharazwa 5-1 na Algeria

April 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MAKINDA wa Kenya waliendelea kufunzwa jinsi ya kusakata soka pale walipepetwa 5-1 na Algeria katika kipute cha Muungano wa Vyama vya Soka vya Kaskazini mwa Afrika (UNAF) Jumatano uwanjani Borg El Arab mjini Alexandria nchini Misri.

Vijana wa kocha Michael Amenga, ambao wamealikwa kushiriki mashindano haya, walizamishwa na mabao kutoka kwa Lotfi Aouane, Chemseddinne Bekkouche, Mohamed Boukerma, Aymen Sais na Belkacem Bouzidad.

Mathew Mwendwa alifungia Kenya bao la kufutia machozi.

Kichapo hiki kiliwasili siku chache baada ya Kenya kupoteza pembamba 1-0 dhidi ya Misri mnamo Aprili 6 katika mechi yake ya ufunguzi.

Mechi ya Kenya ijayo ni dhidi ya majirani Tanzania mnamo Aprili 12 kabla ikamilishe mashindano haya ya mataifa matano dhidi ya Morocco mnamo Aprili 14.

Morocco, Misri na Algeria zimeshinda mechi zao zote kwa hivyo mechi kati ya Kenya na Tanzania huenda ikaamua nani kati yao atavuta mkia.

Vijana wa Amenga walikutana na Tanzania mara ya mwisho Aprili 25 mwaka 2018 katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) nchini Burundi.

Kenya ilichapwa 2-1 katika mechi hiyo ya nusu-fainali.

Tanzania ililima Somalia 2-0 katika fainali na kutawazwa mabingwa.