Michezo

Kenya yachagua 28 wa badminton na para-badminton nchini Misri

Na GEOFFREY ANENE December 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKISHO ya Badminton Kenya na Para-Badminton Kenya Desemba 3, 2025, yaliandaa mashindano ya kuchagua timu ya taifa itakayoshiriki michuano ya Egypt Para-Badminton International itakayofanyika Januari 12–18, 2026 jijini Cairo.

Zoezi ya kuchagua timu hiyo lilifanyika katika ukumbi wa YMCA Shauri Moyo jijini Nairobi, wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu kwa ushirikiano na shirika la kijamii la Women Challenge to Challenge (WCC).

Rais wa Badminton Kenya, Peter Muchiri, alisema kuwa maandalizi ya mapema yatasaidia Kenya kupata mafanikio kama yale ya Mashindano ya Afrika ya Para Badminton 2025 nchini Nigeria, ambako timu ilimaliza nafasi ya pili kwa jumla ya medali 11 (dhahabu nne, fedha mbili na shaba tano).

“Tuna wachezaji wazuri sana, iwe ni wenye uwezo wa kawaida au walemavu, ambao wanaweza kufanya vizuri wakipata usaidizi wa kutosha,” akasema.

Kocha mkuu wa timu ya taifa, John Mburu, alifichua kuwa wachezaji 28 walihudhuria majaribio hayo, na kuwa atachagua kikosi cha mwisho cha wachezaji 20.

Alisema Kenya tayari ina takriban wachezaji wanane wa para-badminton wanaoorodheshwa katika viwango vya ubora duniani, na akasisitiza umuhimu wa kutathmini vipaji vipya kutoka shule za upili na vyuo. “Kwa angaa wiki moja au mbili, nitakuwa nimekamilisha orodha ya muda,” akaongeza.

Miongoni mwa waliohudhuria mashindano kutafuta tiketi ya timu ya taifa na wanatarajiwa kuingia kwenye orodha ya mwisho ni mabingwa wa Afrika Benson Nduva na Anthony Ojwang’. Washindi wengine wa medali waliokuwepo ni Mary Nduku, Boniface Were, Caleb Omollo, Stency Neema, Patrick Muema, Elizabeth Nabwire, Petronila Muhani, Ashley Autai na Newton Gatobu.

Rais wa Shirikisho la Para Badminton Kenya, Jennifer Kamanda, aliwasifu wachezaji na kuzitaka serikali za kaunti kuongeza uwekezaji kwenye miundombinu ya michezo inayowezesha watu wenye ulemavu (PWDs), akisisitiza umuhimu wa huduma jumuishi katika kukuza vipaji.

Zoezi hilo pia lilihudhuriwa na maafisa wa WCC wakiwemo Mkurugenzi Jane Kihungi, Mweka Hazina Jennifer Kamande, Katibu Mkuu Josephta Mukobe na Mwenyekiti Veronica Njuhi, ambao wote walipongeza juhudi zinazoendelea za kuimarisha para-badminton nchini Kenya.