Michezo

Kenya yang’aa Marrakech Marathon Kitwara akivuna Sh1.6 milioni

January 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA GEOFFREY ANENE

MKENYA Sammy Kitwara ameibuka mfalme wa Marrakech Marathon na kujizolea Sh1.6 milioni kwenye mbio hizo zilizovutia washiriki 12,000 nchini Morocco, Jumapili, Januari 28, 2024.

Kitwara amekamilisha mbio hizo za kilomita 42 kwa saa 2:07:53 akifuatiwa kwa karibu na Wamoroko Omar Ait Chitachen na Mustapha Houdadi kwa 2:08:43 na 2:09:36, mtawalia.

Nambari mbili na tatu walitia kibindoni Sh1.1 milioni na Sh650, 596, mtawalia.

Nao, Wakenya Bravin Kiprop na Vincent Kipkorir wamefagia nafasi mbili za kwanza katika mbio za kilomita 21 za Sevilla kwa dakika 59:21 na 59:48 nchini Uhispania, mtawalia.

Mwitaliano Iliass Aouani alifunga tatu-bora kwa saa 1:01:32.

Wakimbiaji tatu-bora mjini Seville walizawadiwa Sh176, 693, Sh132, 520 na Sh88, 346, mtawalia.

Wakenya pia walitawala mbio za Buriram Marathon nchini Thailand mnamo Januari 27, 2024.

Sharon Chelimo (2:27:59), Caroline Jepchirchir (2:30:11) na Sheila Jepkosgei (2:32:11) walifagia nafasi tatu za kwanza za wanawake.

Mathew Samperu (2:09:54), John Mwangangi (2:11:07) na Geoffrey Birgen (2:11:22) walifuatana katika nafasi tatu za kwanza upande wa wanaume, mtawalia.

Watimkaji watatu wa kwanza katika mbio hizo za kilomita 42 mjini Buriram watapokea tuzo ya Sh7.3 milioni, Sh3.2 milioni na Sh1.6 milioni kabla ya kutozwa ushuru mtawalia baada ya matokeo ya kupimwa dawa za kusisimua misuli kutolewa.