Kenya yaomboleza bingwa wa Afrika 3,000m kuruka viunzi na maji Jairus Birech
NAIBU rais wa Shirikisho la Riadha Duniani (WA), Jackson Tuwei, Ijumaa aliongoza taifa kuomboleza kifo cha ghafla cha bingwa wa Riadha za Afrika 2014 katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Jairus Birech.
Birech, ambaye alizaliwa Desemba 14 mwaka 1992, alifariki usiku wa Alhamisi (Septemba 18) baada ya kuugua kwa muda.
Mara ya mwisho alishiriki mashindano ilikuwa katika mbio za Guadalajara Half Marathon nchini Mexico mwaka 2020. Tuwei alimtaja kama mwanariadha mwenye kipaji aliyeletea taifa heshima kubwa.

“Nimesikitishwa sana kupata habari za kifo cha Jairus Birech. Mwenyezi Mungu aipe familia yake yote amani, nguvu na uvumilivu wa kustahimili uchungu huu,” akasema Tuwei ambaye ni rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK).
Mshindi wa medali ya shaba kwenye Olimpiki za London 2012 na bingwa wa dunia 3,000m kuruka viunzi mwaka 2013, Milcah Chemos, pamoja na mshindi wa fedha Olimpiki za Rio 2016 na bingwa wa dunia kurusha mkuki mwaka 2015, Julius Yego, waliungana na wanariadha wenzao kutuma salamu za rambirambi kwa familia.
“Maisha!!! Unajitahidi kuyafanya bora na rahisi kwa familia na watoto wako, halafu ghafla unaondoka jukwaani ukiwaacha wakiwa na huzuni. Lala salama, Jairus! Mtu mnyenyekevu sana aliyekuwa mnyamavu. Angeweza kuongea kwa sauti kubwa tu pale kwenye viunzi! Safiri salama,” aliomboleza Yego.
Majonzi
Kaka yake mdogo, Dennis Kibet, ambaye pia ni mwanariadha, alifichua kuwa Birech alikuwa mgonjwa kwa karibu majuma matatu na kulazwa kwa wiki mbili katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, ambako mwili wake bado umehifadhiwa.
“Tumesikitishwa sana na kifo chake. Si rahisi kumpoteza kaka na mlezi. Tumekuwa hospitalini lakini alipoteza vita usiku wa jana,” aliomboleza Kibet.
Akaongeza: “Birech alipenda sana riadha na baada ya kustaafu mbio za uwanjani alishiriki mbio kadha za barabarani. Aliwapa hamasa na kuwatia moyo wengi, akiwemo mimi, kuingia kwenye riadha. Atakumbukwa sana. Familia na rafiki wataanza kukutana leo (Septemba 19) katika mtaa wa Elgon View na Chebarus, Kesses, kupanga mazishi yake.”