Michezo

Kenya yapoteza mataji ya wanaume na wanawake Paris Marathon

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

Juhudi za Paul Lonyangata kutwaa taji la Paris Marathon kwa mwaka wa tatu mfululizo zimegonga mwamba katika makala ya 43 yaliyoshuhudia Kenya pia ikipoteza mataji ya wanaume na wanawake nchini Ufaransa, Jumapili.

Mkenya Lonyangata, ambaye alikuwa amepigiwa upatu kushinda mbio za kilomita 42 zilizovutia watimkaji 60,000, aliridhika katika nafasi ya tatu. Waethiopia Abrha Milaw na Asefa Mangitsu walifagia nafasi mbili za kwanza kwa saa 2:07:05 na 2:07:25 mtawalia.

Kabla ya mwaka 2019, Kenya ilikuwa imeshinda kitengo cha wanaume cha Paris Marathon kwa miaka minne mfululizo kupitia kwa Mark Korir (2015), Cyprian Kotut (2016) na Lonyangata mwaka 2017 na 2018.

Kenya ilishinda mataji matatu mfululizo kupitia kwa Visiline Jepkesho (2016), Purity Rionoripo (2017) na Betsy Saina (2018) kabla ya kupoteza utawala huo kwa Muethiopia Gelete Burka mwaka 2019. Mkenya wa kwanza kufika utepeni kwa upande wa kinadada mwaka 2019 alikuwa Sally Chepyego katika nafasi ya tano.

Mara ya mwisho Kenya ilikosa mataji ya Paris Marathon kabla ya 2019 ilikuwa mwaka pale Ethiopia ilitawala vitengo vyote viwili.

Matokeo (10-bora):

Wanaume

Abrha Milaw (Ethiopia) saa 2:07:05

Asefa Mangitsu (Ethiopia) 2:07:25

Paul Lonyangata (Kenya) 2:07:29

Morris Gachaga (Kenya) 2:07:46

Barselius Kipyego (Kenya) 2:07:58

Polat Arikan (Uturuki) 2:08:14

Yitayal Atnafu (Ethiopia) 2:08:31

Morhad Amdouni (Ufaransa) 2:09:14

Hillary Kipsambu (Kenya) 2:11:53

Nicolas Navarro (Ufaransa) 2:11:53

Wanawake

Gelete Burka (Ethiopia) saa 2:22:47

Azmera Gebru (Ethiopia) 2:22:52

Azmera Abreha (Ethiopia) 2:23:35

Clemence Calvin (Ufaransa) 2:23:41

Sally Chepyego (Kenya) 2:23:54

Pascalia Kipkoech (Kenya) 2:26:05

Zefrie Limeneh (Ethiopia) 2:26:49