Kenya yateuliwa kupambana na New Zealand, Poland, Palestine, Nicaragua na Peru kuwania taji la Shirikisho Bora la Riadha Duniani
Na CHRIS ADUNGO
SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limeteuliwa kuwania taji la Shirikisho Bora mwanachama wa Shirikisho la Riadha Duniani (WA) almaarufu Member Federation Award kwa ufanisi wa kuandaa mbio za Kip Keino Classic mnamo Oktoba 3.
Riadha hizo zilikokuwa sehemu ya mbio za Dunia za Mabara (World Athletics Continental Tour) zilifanyika katika uwanja wa Nyayo, Nairobi.
AK itashindana na mashirikisho matano mengine wanachama wa WA kwenye tuzo hizo ambapo mshindi atatangazwa rasmi mitandaoni mnamo Disemba 5.
“Licha ya corona kuvuruga ratiba na kalenda ya mashindano mbalimbali ya riadha duniani, AK ilifaulu kuandaa mbio za Kip Keino Classic ambazo zilikuwa za kwanza za kwa mabara ya dunia kufanyika Afrika. Mbali na kutia fora kwenye mashindano hayo, watimkaji wa Kenya walijizolea pia taji la kikosi bora kwenye mbio za Nusu Marathon ya Dunia jijini Gdynia, Poland mwaka huu,” ikasema sehemu ya taarifa ya WA.
Ikitambua juhudi za AK, WA ilipongeza wadau wa riadha wa humu nchini kwa kujituma kiasi cha haja na kufanikisha maandalizi yaliyofana ya mbio za Kip Keino Classic na kuhakikisha kwamba Kenya inawakilishwa kwenye mashindano yote ya haiba kubwa duniani licha ya kuwepo kwa mkurupuko wa corona uliozua kanuni kali za usafiri duniani kote.
“Taji la Member Federation Award mwaka huu linaendea shirikisho ambalo lilifaulu kuinua viwango vya riadha na kuandaa mashindano ya haiba kwa mafanikio makubwa licha ya hali ngumu iliyosababishwa na corona. Sote tunafahamu jinsi corona ilivyotatiza sekta ya michezo duniani mwaka huu,” akasema rais wa WA, Sebastian Coe.
Licha ya changamoto tele za kifedha zilizochangiwa na janga la corona, Wakenya walijituma katika mbio za Kip Keino Classic zilizohudhuriwa na mashabiki 6,000. Mbio hizo zilivutia zaidi ya wanariadha 150 kutoka mataifa 30 tofauti.
Kati ya Wakenya waliotamba katika mbio hizo ni mabingwa wa dunia Hellen Obiri, Timothy Cheruiyot na Beatrice Chepkoech waliotawala vitengo vyao vya mita 5,000, mita 1,500 na mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji mtawalia.
Mbali na AK, wawaniaji wengine wa tuzo hiyo ya kimataifa ni mashirikisho ya riadha nchini New Zealand, Nicaragua, Poland, Peru na Palestine.
“Japo baadhi ya wanariadha wa haiba kubwa zaidi hawakuweza kunogesha mashindano kadhaa yaliyoandaliwa na WA mwaka huu katika sehemu mbalimbali duniani, yapo mashirikisho yaliyojituma pakubwa kiasi cha kuandaa mapambano yaliyohudhuriwa na idadi kubwa ya mashabiki,” ikasema WA.
“Miongoni mwa mashindano hayo ni mbio za Kip Keino Classic nchini Kenya mnamo Oktoba na Rotorua Marathon iliyofanyika New Zealand mnamo Septemba. Hayo ni kati ya mapambano yaliyovutia umma kwa mara ya kwanza tangu Machi,” ikaongeza WA.
Hafla ya kutolewa kwa tuzo za Shirikisho Bora itaandaliwa mnamo Disemba 5, siku ambapo tuzo za Mwanariadha Bora Dunia kwa upande wa wanaume na wanawake pia atatangazwa kupitia mitandao ya YouTube, Twitter na Facebook ya WA.
Wakenya Faith Kipyegon (mita 1,500), Hellen Obiri (mita 5,000) na Peres Jepchirchir (Nusu Marathon) watawania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka wa 2020 kwa upande wa wanawake huku bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500, Timothy Cheruiyot akiwa miongoni mwa watimkaji 10 ambao wameteuliwa kuwania taji hilo kwa upande wa wanaume.
Cheruiyot aliyesajili muda bora wa dunia wa dakika 3:28.45 katika mbio za mita 1,500 mwaka huu, alijivunia rekodi ya kutoshindwa katika fani hiyo baada ya kutawala mbio za Wanda Diamond League katika duru za Monaco (3:28.45) na Stockholm (3:30.25) kabla ya kuandikisha muda wa dakika 3:34.31 katika makala ya Kip Keino Classic.
Ingawa Cheruiyot anapigiwa upatu wa kutwaa taji hilo, atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Joshua Cheptegei wa Uganda ambaye alivunja rekodi za dunia katika mbio za mita 10,000 na mita 5,000. Mwanariadha mwingine anayetarajiwa kumbwaga Cheruiyot ni Mswidi Mondo Duplantis aliyevunja rekodi ya dunia mara mbili katika fani ya kuruka kwa ufito (mita 6.17 na mita 6.18) baada ya kuruka juu zaidi kwenye fani hiyo (mita 6.15) kwenye michezo isiyokuwa ya ukumbini.
Jacob Kiplimo wa Uganda aliyeibuka mshindi wa mbio za dunia za Nusu Marathon mnamo Oktoba 2020 nchini Poland kwa muda wa dakika 58:49 atakuwa pia akiwania tuzo hiyo.
Akina dada watatu wa Kenya watakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Mwingereza Laura Muir, Letesenbet Gidey na Ababel Yeshaneh wa Ethiopia na Sifan Hassan wa Uholanzi. Mwingine ni malkia wa mbio za masafa mafupi raia wa Jamaica, Elaine Thompson-Herah. Hassan ambaye ni mzawa wa Ethiopia, anashikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 10,000 na pia ndiye bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500.