Kerr mwingi wa shukrani kwa kikosi baada ya kuibuka kocha bora Julai
Na CECIL ODONGO
KOCHA wa Mabingwa mara 16 wa KPL Gor Mahia Dylan Kerr amewashukuru wachezaji wake na benchi ya kiufundi kwa kuchangia ushindi wake wa kocha bora, mwezi Julai.
Kwenye sherehe fupi iliyoandaliwa Jumanne katika uwanja wao wa mazoezi wa Camp Toyoyo jijini Nairobi, mkufunzi huyo ambaye hakutarajia kutuzwa wakati huo aliwamiminia sifa kedekede wanadimba wake kwa kushinda mechi zote tano za mwezi huo.
Mkufunzi huyo alipigiwa kura zilizompa ushindi huo na muungano wa wanahabari wa michezo baada ya timu yake kutopoteza mechi yoyote mwezi Juni na kushinda baadhi ya mechi hizo kwa idadi kubwa ya magoli.
Wakati wa sherehe hiyo, Kerr alituzwa kombe pamoja na hundi ya Sh75,000.
“ Lazima nishukuru benchi yangu ya kiufundi kwa usaidizi mkubwa wanaonipa. Wachezaji wangu pia wametia juhudi kubwa tena wa kupigiwa mfano kufanikisha ushindi wa tuzo hii,” akasema Kerr.
Mwezi Juni, K’ogalo waliwaonyesha wapinzani wao kivumbi. Waliwapa Wazito FC kichapo kizito cha 4-0, wakaifunga Nzoia FC 3-1, wakaikalifisha Ulinzi Stars 2-0, wakainyeshea mvua ya magoli Posta Rangers FC 5-0 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya SoNy Sugar FC kwa ushindi wa 1-0.
“Tuliheshimu kila mpinzani tuliyekutana naye mwezi Juni lakini udhabiti na umoja wetu ulitusaidia pakubwa ikizingatiwa kwamba msongamano wa mechi za kuwajibikia katika ratiba ulitulazimu kusakata mechi kila baada ya siku tatu,” akahitimisha Kerr.
Gor Mahia Julai 22 waliendeleza rekodi yao ushindi kwa kuwaangusha watani wao wa jadi AFC Leopards kwa mabao 2-1 kwenye debi ya ‘Mashemeji’ na kufungua mwanya wa alama 12 uongozini mwa KPL (alama 52).
Mpinzani wake aliyeibuka wa pili katika tuzo hiyo alikuwa kocha wa Sofapaka John Baraza.