Michezo

Kesi ya rufaa ya Manchester City dhidi ya marufuku ya Uefa kuanza Juni 8

May 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA CHRIS ADUNGO

KESI ya rufaa ya Manchester City dhidi ya marufuku kusalia nje ya kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kipindi cha miaka miwili ijayo imeratibiwa kuanza Juni 8, 2020, katika Mahakama ya Mizozo ya Spoti Duniani (CAS).

Kesi hiyo itasikilizwa kwa siku tatu mfululizo na matukio hayatawekwa wazi kwa umma kufuatilia. Itaendeshwa kwa njia ya video kutokana na kanuni mpya za sasa zinazodhibiti usafiri kwa sababu ya janga la corona.

Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), walitozwa faini ya Sh3.5 bilioni na kupigwa marufuku ya kushiriki UEFA kwa misimu miwili ijayo mnamo Februari 2020.

Hii ni baada ya kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kupatikana na hatia ya kukiuka sheria za Uefa zinazohusiana na masuala ya matumizi ya fedha na leseni.

Ni matarajio yao kwamba maamuzi hayo huenda yakabatilishwa. Iwapo marufuku itadumishwa, kikosi hicho kitapunguziwa alama katika EPL kwa sababu sheria za udhibiti wa masuala ya fedha katika kivumbi cha EPL kwa kiasi kikubwa, zinawiana na kanuni za Uefa, japo hazifanani moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Sheikh Mansour na Khaldoon Al Mubarak ambao ni wamiliki wa klabu hiyo, hatua ya kuadhibiwa kwao ni jambo la kukatisha tamaa na la kuwapaka tope; ila halijawashangaza sana hasa ikizingatiwa jinsi uchunguzi wa madai yaliyoibuliwa dhidi yao ulivyoendeshwa.

Bodi ya udhibiti wa masuala ya matumizi ya fedha imeshikilia kwamba Man-City walivunja sheria kwa kuweka kiwango cha juu zaidi cha fedha katika mapato yao ya ufadhili kwenye hesabu zao na katika ripoti ya fedha iliyowasilishwa katika afisi za Uefa kati ya mwaka wa 2012 na 2016.

Ripoti zote za Man-City wakati huo zilionyesha kuwa hawakupata hasara wala faida yoyote. Isitoshe, Man-City walidaiwa kutokuwa radhi kushirikiana na maafisa wa Uefa wakati wote wa uchunguzi dhidi yao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na vinara wa Man-City, klabu hiyo imekuwa ikipendekeza kuundwa kwa bodi huru itakayochunguza upya madai dhidi yao kwa uwazi na kufuatwa kwa mchakato usiopendelea upande wowote wakati wa kuangaliwa ushahidi.

“Mnamo Disemba 2018, mchunguzi mkuu wa Uefa alisema wazi vikwazo ambavyo anataka Man-City iwekewe hata kabla ya uchunguzi wenyewe kuanza kufanywa rasmi. Kasoro nyingi na udhaifu mkubwa upo katika mchakato wa uchunguzi wa Uefa. Hakukuwa na shaka kwamba matokeo ya uchunguzi huu yangeishia kuwa hivi: sisi kupigwa marufuku na kutozwa faini. Klabu hii awali ilikuwa imewasilisha malalamiko yake kwa bodi ya nidhamu ya Uefa, ambayo yaliidhinishwa na mahakama ya kusuluhisha migogoro ya michezo,” ikatanguliza.

“Hii ni kesi iliyowasilishwa na Uefa, ikashtakiwa na Uefa na aliyetoa uamuzi ni Uefa. Kwa mchakato wa kibaguzi aina hii ambao umemalizika, klabu hii sasa itatafuta hukumu ya waamuzi wasiopendelea upande wowote haraka iwezekanavyo. Ingawa hivyo, kwanza kabisa, itaendelea na mchakato wake katika mahakama ya kusuluhisha migogoro ya michezo bila kuchelewa,” ikasema sehemu nyingine ya taarifa hiyo.

Rais wa La Liga Javier Tebas, tayari ameisifu Uefa kwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya Man-City.

“Adhabu hiyo itahakikisha kwamba kuna utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa fedha na kutoa jukwaa la kudhibitiwa vilivyo wanaokiuka sheria hiyo. Hili ni jambo la msingi litakalotoa mwongozo bora kwa mpira wa kandanda ambao kwa sasa unatawaliwa na ulaghai,” akatanguliza.

“Kwa miaka mingi, tumekuwa tukitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua mwafaka dhidi ya klabu za Man-City na Paris Saint-Germain (PSG), na hatimaye tumepata mfano bora. Ni matumaini yetu kwamba hili litaendelezwa zaidi na wengi watapata kujifunza. Ni heri kuchelewa kuliko kutochukuliwa kabisa kwa hatua yoyote,” akasisitiza Tebas.