Michezo

Kevin De Bruyne atawazwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa PFA

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KIUNGO Kevin De Bruyne wa Manchester City ametawazwa Mwanasoka Bora wa Kiume wa Mwaka na Chama cha Wanasoka (PFA).

Nyota huyo mzawa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 29, amemsifu kocha Pep Guardiola kuwa nguzo na kiini cha ufanisi huo kwa kusisitiza kuwa ni mkufunzi ambaye amemruhusu “kucheza soka kwa mtindo aupendao na katika nafasi inayomridhisha zaidi ugani”.

Beth England, 26, aliibuka mshindi kwa upande wa wanawake baada ya kusaidia Chelsea kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (Women’s Super League) na taji la League Cup katika msimu wa 2019-20.

Beki Trent Alexander-Arnold wa Liverpool alitawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka. Nyota huyo mzawa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 21, aliwabwaga Tammy Abraham (Chelsea), Marcus Rashford, (Manchester United), Mason Greenwood (Manchester United), Mason Mount (Chelsea) na Bukayo Saka wa Arsenal.

Jordan Henderson alikuwa miongoni mwa wanasoka watano wa Liverpool waliojumuishwa katika Kikosi Bora cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wa 2019-20.

Fowadi Marcus Rashford wa Manchester United alitawazwa Mwanasoka wa Hisani kubwa miongoni mwa wachezaji wanachama wa PFA kwa ukubwa wa mchango wake katika kukabiliana na umaskini, kutetea haki za watoto na kuwapa chakula.

De Bruyne alimpiga kumbo mshindi wa tuzo hiyo mwaka jana, Virgil van Dijk wa Liverpool pamoja na Alexander-Arnold, Sadio Mane, Henderson na Raheem Sterling ambaye ni mwenzake kambini mwa Man-City.

Mbelgiji huyo anakuwa mwanasoka wa kwanza wa Man-City kutwaa taji hilo tangu tuzo hiyo iasisiwe mnamo 1973-74.

Kwa mwaka wa tatu mfululizo, taji la Mwanasoka Bora wa Mwaka linamwendea mchezaji ambaye kikosi chake hakikuibuka mshindi wa kivumbi cha EPL.

Van Dijk alipokezwa taji hilo mwaka jana baada ya mwenzake wa Liverpool, Mohamed Salah kutuzwa mwishoni mwa msimu wa 2017-18. Katika misimu hiyo miwili, Liverpool waliambulia nafasi za pili nyuma ya Man-City walionyanyua ufalme wa taji la EPL.

Licha ya kuweka rekodi kwa kuchangia mabao 20 na kufunga mengine 13 akivalia jezi za Man-City mnamo 2019-20, ushawishi wa De Bruyne haukuwezesha Man-City kuwapiku Liverpool katika vita vya kuwania ubingwa wa taji la EPL. Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walitawazwa mabingwa w akipute hicho kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 ya kusubiri.

Kwa upande wake, England alifungia Chelsea jumla ya mabao 21 katika mashindano yote ya msimu wa 2019-20 na kumbwaga Vivianne Miedema wa Arsenal. Hii ni mara yake ya pili mfululizo kutawazwa taji la Mwanasoka Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake.

Mbali na Miedema, aliwaangusha pia Sophie Ingle na Guro Reiten wa Chelsea na Ji So-yun wa Arsenal.

KIKOSI BORA CHA EPL MSIMU WA 2019-20:

Nick Pope (Burnley), Trent Alexander-Arnold, Virgil van Dijk (both Liverpool), Caglar Soyuncu (Leicester), Andrew Robertson (Liverpool), David Silva (Manchester City), Jordan Henderson (Liverpool), Kevin de Bruyne (Manchester City), Jamie Vardy (Leicester), Pierre-Emerick Aubameyang (Arsenal), Sadio Mane (Liverpool).