Michezo

KHN yapiga Zetech, Balaji yaibuka kidedea

July 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA JOHN KIMWERE

TIMU ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) iliandikisha ufanisi wa mabao 2-0 dhidi ya Zetech University na kuibuka ya pili huku Balaji EPZ ikichoma Magana Flowers magoli 3-1 na kutwaa ubingwa wa mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu.

Ili KNH kubeba taji hilo ilihitaji kushinda wapinzani wao nayo Balaji EPZ itoke nguvu sawa ama ipoteze mchezo huo.

Licha ya kocha wa Zetech University, Bernard Kitolo kujipiga kifua vijana wake wangefanya kweli walikosa ujanja na kujipata hoi mbele ya KNH iliyokuwa katika ardhi ya nyumbani.

KNH ilinasa ushindi huo baada ya Ben Obiri (nahodha) na Brian Otieno kila mmoja kuitingia bao moja. ”Dah! Hali siyo hali, kwa mara nyingine tumaini letu limegonga mwamba, hata hivyo nawashukuru sana wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliofanya msimu huu,” kocha wa KNH, George Makambi alisema na kuongeza kuwa wamebaki roho maana hawaelewi kama watapata nafasi ya kupanda ngazi muhula ujao.

Wanasoka wa KNH wanaonekana wanazidi kuimarika baada ya kumaliza nafasi ya nne na tatu kwenye msimu wa 2017 na 2018 mtawalia.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Uweza FC ililazimika kutoka nguvu sawa mabao 3-3 na Limuru Olympics.

Balaji EPZ imenasa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu ujao.

Balaji EPZ iliibuka kidedea kwa alama 46, moja mbele ya KNH. Nayo Zetech University ilifunga tatu bora kwa alama 40, moja mbele ya Uweza FC huku Limuru Olympic ikitua tano kwa alama 38.