Michezo

Kibera Saints yararua Riruta United magoli 4-2

October 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

KIBERA Saints ilikung’uta Riruta United kwa magoli 4-2 katika mchezo wa kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) ulioandaliwa uwanjani NCC jijini Nairobi.

Nayo Uweza B FC iliangukia pua kwa kushindwa magoli 3-0 na maafande wa Nairobi Prisons katika patashika iliyochezewa ugani Nairobi Prisons.

Saints ilipata mafanikio hayo kupitia Isaac Kimonyi aliyefunga mara mbili, huku Kevin Omondi na Felix Ochieng kila mmoja akicheka na wavu mara moja.

Nao Simon Mureithi na Joseph Nandwa kila mmoja alitingia Riruta bao moja.

Nairobi Prisons iliyoibuka ya pili katika msimamo wa kipute hicho Kundi A msimu uliopita ilinasa pointi zote muhimu kutokana na mabao ya Gabriel Nyambari, Cephans Ojogo na Yusuf Lussinga kila mmoja alipotinga moja.

”Tunapania kuendeleza mtindo huo kwenye mechi zijazo maana tunataka tiketi ya kusonga mbele,” kocha wa Kibera Saints, William Mulatya alisema na kuongeza kuwa wanaamini watafanya kweli msimu huu.

Alidokeza kuwa baada ya kuteleza na kumaliza nafasi ya tano msimu uliopita, raundi hii wanalenga kuibuka miongoni mwa nafasi mbili za kwanza kwenye jedwali.

Kibera Saints inajivunia kurejea kwa straika Enock Omosa aliyekuwa akipigia Uweza FC kwa mkopo.

Pia wametwaa huduma za beki Boaz Omondi (Azuri FC) na Kevin Omondi (Gorp FC).

Vilevile, wamepandisha Brian Emori kutoka timu ndogo kwa wasiozidi umri wa miaka 17.