Kibera Utd, Ruiru Hotstars kusaka ubabe Daraja la Pili
Na JOHN KIMWERE
KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa kwenye mechi za kuwania tiketi za kufuzu kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza muhula ujao. Michuano hiyo ya kupigania tiketi mbili za kusonga mbele inatarajiwa kuandaliwa baada ya janga la Corona itakapojumuisha jumla ya timu sita za Ligi ya Taifa Daraja la Pili.
Mlipuko huo ulichangia shughuli za michezo nchini kupigwa stopu tangu mwezi Machi mwaka huu. Ligi ya Taifa Daraja la Pili imegawanywa mara tatu Kundi A, B na C ambapo timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitakutanisha kucheza fainali ya kusaka bingwa wa ngarambe hiyo.
Ruiru Hotstars na Kibra United ni miongoni mwa timu zinazoratibiwa kushuka dimbani kusaka ubabe wa kufuzu kushiriki kipute hicho.
Vikosi hivyo vilimaliza kati ya nafasi mbili bora kwenye mechi za mkumbo wa kwanza Kundi A. Kibra chini ya nahodha, Nassor ‘Alolo’ Yusuf iliibuka ya pili kwa kukusanya alama 29 baada ya kuingia dimbani mara 13. Nayo Ruiru Boys ilimaliza kileleni kwa kutia kapuni pointi 29 tofauti ikiwa idadi ya magoli.
”Tunatarajia kibarua kigumu dhidi ya wapinzani wetu kwenye juhudi za kutafuta tiketi ya kusonga mbele,” alisema kocha wa Kibra United, Caleb Arunga na kuongeza kuwa ana imani tosha wachezaji wake wana uwezo tosha kuvuruga wapinzani wao na kufanikiwa kubeba tiketi ya kupandishwa ngazi.
Kibra iliyomaliza ya kumi msimu uliyopita ilionekana kuja kivingine muhula huu kutokana na juhudi za wanyakaji wake matata akiwa Edward Apuk, Malik Omondi na Moses Ndambuki.
Meneja wake, Said Rajab anasema kando na wachana nyavu hao pia kikosi hicho kinajivunia huduma za baadhi ya wachezaji wazoefu waliokuwa mstari wa mbele kukivumisha msimu huu.
Kibra inajivunia kukuza wachezaji wengi tu waliwahi kupigia klabu mbali mbali hapa nchini. Baadhi yao wakiwa: Habib Mohammed, Mohammed Hassan, Augustine Omondi, Charles Ouma na Ramadhan Iddi (Ligi Ndogo).
Timu hii ilibuniwa miaka minane iliyopita dhamira kuu ikiwa kutumia soka kuleta vijana pamoja kusudi kuwaepusha dhidi ya kushiriki matendo maovu mitaani. Pia waanzilishi walipania kufundishwa wachezaji wake masuala tofauti ya kijamii kuhusiana na maisha ya miaka ya sasa.
Kundi hilo lilishirikisha klabu 14 zikiwamo:Ruiru Hotstars, Kibra United, Gogo Boys, Butterfly FC marufu King of Ruiru, Kariobangi Sharks 11, Nyahururu Griffon, Korogocho Youth, CMS Allstars, South B Sportiff, Tusker Youth, Nanyuki Youth, Utafiti FC, Vision FC ma South B Allstars.