KIGEZONI: Manchester City, Spurs nguo kuchanika
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
UWEZO wa Manchester City kutetea taji la Ligi Kuu ya Uingereza unatarajiwa kupimwa vilivyo na Tottenham Hotspur leo Jumamosi uwanjani Etihad.
City ya kocha Pep Guardiola ilifungua kampeni yake msimu huu kwa kuwaaibisha West Ham 5-0 ugenini kupitia mabao ya Raheem Sterling (3), Sergio Aguero (penalti) na Gabriel Jesus.
Spurs ambayo ilishinda Ligi Kuu mara ya pili na mwisho msimu 1960-1961, pia ilianza vyema kwa kupiga washiriki wapya Aston Villa 3-1 japo kwa jasho baada ya kutoka nyuma na kuzoa alama tatu kupitia mabao ya Harry Kane (mawili) na sajili mpya Tanguy Ndombele.
John McGinn alifungia Villa bao la mapema kabla ya Spurs kujibu na mabao hayo katika dakika 17 za mwisho.
Timu zote zinaingia mchuano huu na motisha ya juu. Hata hivyo, safari ya Spurs uwanjani Etihad katika mechi tatu zilizopita haijakuwa nzuri.
Ilitwangwa 4-1 mwaka 2017 na 1-0 mwezi Aprili 20 mwaka huu katika mechi za ligi na kulemewa 4-3 katika Klabu Bingwa Ulaya mnamo Aprili 17, 2019.
City pia inajivunia rekodi ya kutoshindwa na Spurs uwanjani Etihad katika mechi tatu za ligi zilizopita.
Itatumai kuendeleza rekodi hii baada ya kufungua msimu kwa kuonyesha dalili haijapoteza makali yaliyoifanya kufagia mataji ya Ligi Kuu, Kombe la FA na League Cup msimu uliopita.
City kuamka
Kuna wakati City ilionekana dhaifu dhidi ya West Ham, hasa baada ya kuongoza 2-0, lakini ikaamka tena na kupata mabao matatu katika dakika 15 za mwisho.
Sterling, ambaye alimiminiwa sifa tele kwa mchango wake wa mabao matatu katika kipindi cha pili cha mechi hiyo, ni mmoja wa wachezaji watakaotegemewa na City kuamua mwelekeo wa mechi hii yao ya 160 dhidi ya Spurs.
Mwingereza huyu amefunga mabao manne dhidi ya Spurs katika mechi tatu zilizopita uwanjani Etihad.