Kijiji cha Kapsisiywa kunufaika kutokana na jasho la Eliud Kipchoge
Na GEOFFREY ANENE
MAELFU ya wakazi wa kijiji cha Kapsisiywa wanatarajiwa kunufaika pakubwa kutokana na jasho la Eliud Kipchoge baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza ufadhili wa Sh100 milioni kwa ujenzi wa shule na maktaba kwa heshima ya mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya marathon ya wanaume.
Kijiji hiki kinapatikana katika eneobunge la Emgwen katika kaunti ya Nandi. Kina shule kadhaa zikiwemo zile za msingi na sekondari Kapsisiywa.
Waziri wa Elimu, George Magoha alifika katika kijiji hicho anakotoka Kipchoge siku ya Ijumaa na kutoa hundi ya Sh100 milioni, huku akifichua kuwa Rais Kenyatta ameahidi kuzuru shule hiyo miezi sita ijayo.
“Rais Kenyatta ametangaza ufadhili wa Sh100 mililioni kwa ujenzi wa maktaba mpya kwa heshima ya makubwa ambayo Kipchoge amefanyia Kenya,” Magoha alisema.
Kipchoge, ambaye anayeshikilia rekodi rasmi ya mbio za kilomita 42 za wanaume ya saa 2:01:39 aliyoweka jijini Berlin nchini Ujerumani mwaka 2018, aliandikisha historia ya kuwa mtu wa kwanza kukamilisha umbali huo duniani chini ya saa mbili alipotimka mbio za INEOS 1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 jijini Vienna nchini Austria mnamo Oktoba 12, 2019.
Muda huu haukutambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kama rekodi ya dunia kwa sababu zilikuwa mbio maalum, ambazo hakushindana na mtu.
Magoha alitoa onyo kali kwa maafisa watakaojaribu kufuja fedha hizo akisema watapigwa kalamu.
Waziri huyo alifichua kuwa Rais Kenyatta aliitikia mwito wa Kipchoge kumtaka ajenge maktaba mpya na shule katika kijiji hicho chake.