Michezo

Kikosi cha Gor kitakachosafiri Algeria chatajwa

August 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

MABINGWA  wa KPL Gor Mahia, wametaja wachezaji 17 watakaokamilisha kikosi  kitakachosafiri hadi taifa la Algeria kuchuana na USM Alger Jumatano, Agosti 29 katika  mechi ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho, CAF.

K’Ogalo wanatarajiwa kuondoka Jumatatu Agosti 27 kuchuana na mibabe hao wa soka ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini wakilenga angalau kupata sare ili kufuzu hatua ya robo fainali ya kidumbwedumbe hicho.

Difenda matata Karim Nzigiyimana ambaye alirejea kikosini baada ya kuwa nje kwa kipindi cha mwaka moja na kipa tegemeo Fredrick Odhiambo ni miongoni mwa wanadimba waliojumuishwa katika kikosi hicho.

Odhiambo ambaye awali alikuwa kipa nambari tatu alionyesha mchezo wa hali ya juu katika ushindi  wa 3-0 dhidi ya  mabingwa wa KPL mwaka wa 2009 Sofapaka  mjini Narok  Agosti 23 na wa 2-0 katika debi ya Mashemeji dhidi ya AFC Leopards iliyosakatwa ugani MISC Kasarani Jumamosi  Agostti 25.

Kutokana na kuimarika kwa kiwango chake  na kung’aa kwenye mechi hizo, chipukizi huyo sasa amewapiga kumbo langoni  makipa Boniface Oluoch na Shaban Odhonji na kutwaa mikoba ya kipa nambari moja au mlinda lango wa kwanza.

Hata hivyo Odhoji, milinzi Wellington Ochieng’ na mshambulizi Ephraim Guikan anayeuguza jeraha hawajatajwa kikosini na kwa hivyo hawatashiriki mechi hiyo.

Kikosi kamili

Bonface Oluoch, Fredrick Odhiambo, Haron Shakava, Joash Onyango, Wesley Onguso, Karim Nzigyimana, Ernest Wendo, Humphrey Mieno, Bernard Ondiek, Lawrence Juma, Francis Kahata, George Odhiambo, Samuel Onyango, Jacques Tuyisenge, Francis Mustapha, Charles Momanyi, Philemon Otieno.