Michezo

Kikosi cha Ujerumani chapepetwa 37-0 !

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KIKOSI cha Ripdorf nchini Ujerumani kilipokezwa kichapo cha 37-0 kutoka kwa SV Holdenstedt II baada ya kuchezesha wanasoka saba pekee ili kutimiza kanuni ya kukabiliana na msambao wa virusi vya corona.

Kwa kipindi kizima cha dakika 90, kikosi hicho kilicheza kwa kudumisha umbali wa mita moja na zaidi kati ya mwanasoka uwanjani.

Hatua ya Ripdorf ya kupanga wachezaji saba pekee katika kikosi chao ilichochewa na ripoti kwamba wapinzani wao Holdenstedt walikuwa wametangamana na mtu mmoja aliyekuwa akiugua ugonjwa wa Covid-19 kabla ya mchuano huo kuanza.

Ingawa vipimo ambavyo vikosi vyote viwili vilifanyiwa kabla ya mechi vilibaini kwamba hakuna yeyote aliyekuwa na corona wakati wa kusakatwa kwa mechi hiyo, Ripdorf walisisitiza kwamba hawakuwa na imani na vipimo hivyo na walihisi kwamba “haikuwa salama kwao kukaribiana sana ugani”.

Aidha, walihoji kwamba siku 14 hazikuwa zimekamilika baada ya wanasoka wao na wale wa kikosi kizima cha Holdenstedt kufanyiwa vipimo vya corona.

Iwapo Ripdorf wangesusia mchuano huo wa Ligi ya Daraja la 11 nchini Ujerumani, basi wangetozwa faini ya Sh25,500 ambazo walisema hawakuwa radhi kutoa.

Awali, walikuwa wamomba mechi hiyo iahirishwe ila wasimamizi wa Shirikisho la Soka la Ujerumani wakatupilia mbali ombi lao.

Ripdorf walishikilia kwamba hofu yao zaidi ilichangiwa na hatua ya wapinzani wao kuwajibisha kikosi cha pili badala ya wanasoka wao tegemeo katika kikosi cha kwanza.

Mwanzoni mwa mechi, mwanasoka mmoja wa Ripdorf alielekea katikati ya uwanja, akagusa mpira na kumpokeza mpinzani wake kabla ya kuelekea pembezoni ma uwanja kuungana na wachezaji wenzake.

“Wachezaji wa Holdenstedt hawakutaka kutuelewa. Hata hivyo, tusingetaka kabisa kuhatarisha maisha ya wanasoka wetu ambao hawakutaka kuwania mpira kutoka kwa wapinzani na pia wakadumisha umbali wa zaidi ya mita moja na nusu kati yao,” akasema Mwenyekiti wa Ripdorf, Patrick Ristow katika mahojiano yake na ESPN.

“Licha ya hali, maamuzi na msimamo wetu, wapinzani wetu hawakuhisi chochote wala kutuonea imani. Walifunga bao kila baada ya dakika mbili au tatu.

Kwa upande wake, kocha Florian Schierwater wa Holdenstedt alisema kwamba wapinzani wao hawakuwa na sababu wala misingi yoyote ya kutoshiriki mchuano wao kikamilifu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO