• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Kilio huko Man U wakipoteza mechi waliyokuwa wanashinda ndani ya dakika mbili

Kilio huko Man U wakipoteza mechi waliyokuwa wanashinda ndani ya dakika mbili

LONDON, Uingereza

BRUNO Fernandes amelia kuwa Manchester United ililala ikizamishwa 4-3 na Chelsea hapo Alhamisi ugani Stamford Bridge kupitia bao la dakika ya 111 licha ya kufahamu wenyeji wanapenda kupiga kona za haraka.

Katika siku ambayo mahasimu wao wa tangu jadi Liverpool waling’oa Arsenal kileleni mwa jedwali kwa kulima wavuta-mkia Sheffield United ugani Anfield, Fernandes alichemka baada ya Cole Palmer kufunga penalti na bao la ushindi kutokana na kona ya haraka.

United ya kocha Erik ten Hag ilisukumiwa makombora 28 katika mchuano huo baada ya makombora zaidi ya 100 kuelekezwa katika lango lake katika mechi nne zilizotangulia.

Nahodha Fernandes alisikitika kuwa safu ya ulinzi ya United inavuja sana na kukasirishwa hata zaidi kuwa timu hiyo inafahamu mchezo wa Chelsea hutumia kona za kuchanjwa haraka, lakini haikuzuia bao la ushindi.

“Hii mechi ilikuwa mikononi mwetu na tukaitupa. Inasikitisha. Inauma sana. Tulidhibiti mechi vizuri katika dakika za lala salama. Hata hivyo, walipata nafasi mbili na kuzitumia vyema. Tunafaa kujipanga haraka kona inapopatikana. Tulifahamu mapema kuwa wanapiga kona za haraka na pia kutupa mipira kwa haraka,” akasema Mreno huyo.

Aliongeza, “Katika mechi kadhaa zimepita, tumesukumiwa makombora mengi sana. Nadhani hatulindi kisanduku chetu vyema.”

Chelsea iliongoza 2-0 kupitia Conor Gallagher dakika ya nne na penalti ya Palmer dakika ya 19. Hata hivyo, United ilichukua uongozi 3-2 baada ya kupata mabao kutoka kwa Alejandro Garnacho (dakika ya 34 na 67) na Fernandes (39).

Vijana wa kocha Mauricio Pochettino kisha walisawazisha 3-3 dakika ya 110 kupitia penalti nyingine ya Palmer aliyegonga msumari wa mwisho dakika moja baadaye kutokana na kona.

Kilio cha United kinakuja wakati Liverpool imejaa motisha kabla ya ziara ya Old Trafford hapo Jumapili baada ya kupasha misuli moto kwa kucharaza Sheffield 3-1 kupitia magoli ya Darwin Nunez (17), Alexis Mac Allister (76) na Cody Gakpo (90). Sheffield walipata bao la kufuta machozi kutoka kwa Conor Bradley aliyejifunga dakika ya 58.

United waliopiga vijana wa Jurgen Klopp 4-3 na kuwabandua kwenye Kombe la FA mnamo Machi 17, bado hawajaonja ushindi tangu ligi irejee baada ya mechi za timu za taifa za Fifa. Walikabwa 1-1 na Brentford mnamo Machi 30.

“Ni mechi kubwa dhidi ya Liverpool hapo Jumapili. Sidhani nafaa kuambia wachezaji wenzangu chochote. Kama nafaa kusema chochote, basi ni kuwa kuna shida kwa sababu hii ni klabu kubwa,” akasema Fernandes.

Mabao mawili ya Garnacho, 19, yalimfanya kuwa tineja wa kwanza tangu msimu 1998-1999 kupata mabao mawili mara tatu katika msimu mmoja wa Ligi Kuu. Ni rekodi iliyoshikiliwa na Michael Owen akiwa Liverpool.

Leo itakuwa zamu ya Arsenal (pointi 68) na Manchester City (67) kujaribu kung’oa Liverpool (70) kileleni watakapozuru Brighton na Crystal Palace, mtawalia.

Ratiba: Aprili 6 – Crystal Palace vs Manchester City (2.30pm), Wolves vs West Ham (5.00pm), Everton vs Burnley (5.00pm), Aston Villa vs Brentford (5.00pm), Fulham vs Newcastle (5.00pm), Luton Town vs Bournemouth (5.00pm), Brighton vs Arsenal (7.30pm); Aprili 7 – Manchester United vs Liverpool (5.30pm), Sheffield United vs Chelsea (7.30pm), Tottenham vs Nottingham Forest (8.00pm).

  • Tags

You can share this post!

Wamekwepa skendo na drama licha ya kuweka penzi hadharani

Biden aendelea kumchoka kabisa Netanyahu kwa jinsi...

T L