Michezo

KILIO TU: Atletico Madrid yaizidi nguvu Liverpool

March 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL, Uingereza

KOCHA Jurgen Klopp amekiri kuudhika na soka ya Atletico Madrid, baada ya Wahispania hao kubandua nje vijana wake wa Liverpool kutoka kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Jumatano.

Kocha huyo Mjerumani alishuhudia vijana wake wakilemewa 3-2 uwanjani Anfield usiku wa Jumatano, na kuyaaga mashindano hayo ya kifahari kwa kushindwa kwa jumla ya mabao 4-2.

Mabingwa hao watetezi walikuwa wamepoteza 1-0 katika mkondo wa kwanza mjini Madrid, mnamo Februari 18.

Klopp hakuficha jinsi alikeketwa na mchezo wa Atletico, akisema mbinu walizotumia Wahispania hao kulinda ngome yao zilimkera sana. Baada ya mechi alipongeza vijana wake, ingawa pia hakujizuia kutupia Atletico cheche za maneno.

“Jinsi wanavyocheza, siwaelewi. Sielewi jinsi baadhi ya wachezaji bora duniani wanaweza kusakata soka kama hiyo,” alisema bila kufafanua nini hasa kilichomuudhi katika mtindo wa wapinzani.

“Pongezi Atletico, lakini nimeshangazwa na tulivyopoteza. Siwezi kusema zaidi ya hapo kwa sababu nitaonekana kama mshindani asiyekubali kushindwa!”

Kwa upande wake, kocha Diego Simeone alikiri kuwa vijana wake wa Atletico walibahatika kutoka uwanjani Anfield na ushindi.

“Ilikuwa (ushindi) katili kwa sababu tulikuwa na nusu saa ya ziada kufunga mabao matatu ugenini, hapa uwanjani Anfield, na hiyo si haki,” alisema raia huyo wa Argentina.

Mholanzi Georginio Wijnaldum alifungia Liverpool bao la pekee katika muda wa kawaida wa dakika 90, na kufanya timu hizo kuwa na jumla ya mabao 1-1 katika mikondo miwili. Hii ilimaanisha mechi lazima iende dakika 30 za nyongeza ili kuamua mshindi.

Mbrazil Roberto Firmino aliongeza matumaini ya Reds kusonga mbele alipofuma wavuni bao la pili dakika ya 94.

Zikisalia dakika 16 mchuano utamatike, Liverpool walikuwa wamefanya ya kutosha kuingia robo-fainali. Walikuwa juu mabao 2-0 na hivyo kifua mbele kwa jumla ya mabao 2-1.

Lakini masihara ya kipa Adrian na pia kazi safi ya mlinda lango mwenza wa Atletico, Jan Oblak ziliwanyima Waingereza hao tiketi.

Marcos Llorente, ambaye alijaza nafasi ya Mhispania mwenzake Diego Costa dakika ya 56, aliona lango kunako dakika ya 97 na kufanya mechi kuwa 1-2; hivyo kusawazisha kipute kwa jumla kuwa 2-2.

Muda si muda aliongeza bao lake la pili dakika ya 105 na kufanya mambo 2-2, jumla ya mabao ikawa 3-2 kwa faida ya Atletico.

Straika Alvaro Morata alizamisha chombo cha Liverpool zikisalia sekunde chache kipenga cha mwisho kilie.

Mechi ikaisha 3-2 huku kipute hicho kikikamilika kwa jumla ya mabao 4-2 kwa faida ya Atletico.

Liverpool sasa wameshuhudia ndoto yao ya kutetea taji la UEFA na pia kuwania makombe ya FA na Carabao ikizimwa ndani ya siku 12.

Wamesalia katika shindano moja pekee msimu huu – Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ambako wanaselelea kileleni wakiwa na nafasi kubwa kutawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza katika miaka 30.

Wako na mwanya wa pointi 25 kati yao na nambari mbili, Manchester City mechi zikisalia tisa.