Kimanzi aahidi kuvumisha Harambee Stars
Na CECIL ODONGO
KOCHA mpya wa Harambee Stars, Francis Kimanzi ameahidi kutambisha timu hiyo atakapokuwa usukani huku akiahidi kushirikiana na wadau wote kwenye fani ya kabumbu kufanikisha azimio hilo.
Kimanzi ambaye atatambulishwa leo Ijumaa na kupokezwa kazi hiyo rasmi na Shirikisho la Soka Nchini (FKF), anatarajiwa kushirikiana na naibu kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno kwenye ukufunzi baada ya Sebastien Migne kujiuzulu wadhifa huo kwa makubaliano na shirikisho hilo Jumanne.
“Ni fahari kuu kurejea katika timu ya taifa kama kocha mkuu. Nimekuwa hapa awali na ninafahamu vyema majukumu yanayoandamana na kazi hii. Niko tayari kutekeleza wajibu wangu kikamilifu na kuhakikisha kuwa timu inavuma zaidi kwa kupiga hatua kwenye mashindano muhimu,” akasema Kimanzi.
Aidha, kocha huyo wa zamani wa timu za Mathare United na Tusker FC, alisema kuwa anafahamu timu hiyo kwa undani kwa kuwa alishirikiana na Migne japo kilichosalia pekee ni kujenga msingi imara na kurejesha matumaini ya mashabiki kwenye kikosi cha taifa.
“Nilikuwa na mlahaka mwema na Migne. Nilikuwa chini yake na tulishirikiana pamoja kufanya maamuzi muhimu kuhusu timu yetu. Ni wakati wangu sasa wa kuimarisha msingi tuliouweka na nitahakikisha ninawajibika,” akaongeza Kimanzi.
Aidha, alishikilia kwamba atashirikiana na Zico ambaye alijizolea sifa kedekede kama naibu kocha wa mabingwa mara 18 wa Ligi Kuu (KPL), Gor Mahia kabla ya kuhamia KCB kama kocha mkuu miezi miwili iliyopita.
“Tumefahamiana na Zico kwa muda mrefu kwenye fani hii ya soka na nina wingu la matumaini kuwa tutashirikiana kwa lengo la kuboresha soka ya taifa hili. Ombi langu kwa mashabiki ni kuunga timu jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya na ninawahakikishia kuwa sisi tunawajibika vilivyo,” akasema.
Makocha wazawa
Pia aliwataka mashabiki kuunga makocha wazawa badala ya kuamini kwamba timu inaweza kuvuma kupitia ukufunzi wa makocha wa kigeni.
Kibarua cha kwanza cha Kimanzi ni mwezi Novemba ambapo Harambee Stars itagaragazana na timu ya taifa ya Misri kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Afrika(AFCON) mwaka wa 2021.
Akigusia mechi hiyo, Kimanzi aliwaondolea mashabiki hofu kwamba kundi la Kenya linalojumuisha pia Togo na Kisiwa cha Ngazija (Comoros) ni gumu, akisema hakuna lisilowezekana katika mchezo wa kandanda.
“Tulifuzu kwa Afcon ya 2019 na tutajitahidi tusikose makala yajayo ya mwaka 2021,” akasema kocha huyo.