• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kimanzi hana kazi Harambee Stars

Kimanzi hana kazi Harambee Stars

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limeagana rasmi na kocha wa Harambee Stars, Francis Kimanzi mwaka mmoja tu baada ya mkufunzi huyo wa zamani wa Tusker FC na Mathare United kuaminiwa fursa ya kuwa mrithi wa Mfaransa Sebastien Migne.

Katika taarifa yake Jumanne, FKF ilisema kwamba Kimanzi, kwa pamoja na waliokuwa wasaidizi wake kambini mwa Stars, walikatiza uhusiano wao na shirikisho kwa maelewano.

Miongoni mwa maafisa hao ni aliyekuwa msaidizi wa Kimanzi, Zedekiah ‘Zico’ Otieno na mkufunzi wa makipa Lawrence Webo waliokuwa sehemu ya benchi ya kiufundi iliyoongoza Stars kushiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15.

“FKF inashukuru Kimanzi na maafisa waliokuwa wakihudumu naye kwenye benchi ya kiufundi kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika timu ya taifa kwa kipindi ambacho wamekuwa nasi,” ikatanguliza taarifa hiyo iliyotiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno.

“Kimanzi amekuwa kocha wa haiba ambaye amefanya kazi kwa kujitolea na kwa utaalamu mkubwa. Chini ya ukufunzi wake, Stars walikuwa walidhihirisha kiwango kikubwa cha kuimarika kiasi cha kuwa pazuri zaidi kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON 2021 na Kombe la Dunia 2022.”

Fainali hizo zimepangiwa kufanyika nchini Cameroon na Qatar mtawalia.

Kwa mujibu wa Otieno, hakuna ufafanuzi wowote mwingine utakaotolewa na FKF hadi pale ambapo shirikisho litamwajiri mkufunzi mpya wa Stars katika kipindi cha wiki chache zijazo.

Kimanzi anajivunia tajriba pana akidhibiti mikoba ya Stars hasa ikizingatiwa kwamba aliwahi kudhibiti mikoba ya kikosi hicho kwa vipindi viwili tofauti kati ya Novemba 2008 na Januari 2009 kisha Novemba 2011 hadi Juni 2012.

Zico aliwahi pia kuwatia makali masogora wa Stars kati ya Disemba 2010 na Disemba 2011. Kinachosubiriwa kwa sasa ni iwapo atasalia kuhudumu kama kocha mkuu wa wanabenki wa KCB au atajiuzulu kwenye wadhifa huo aliopokezwa mnamo Juni 2019 baada ya kubanduka kwa Frank Ouna.

Kimanzi na wasaidizi wake kambini mwa Stars wanavunja ndoa na FKF siku chache baada ya Nick Mwendwa kuhifadhi kiti cha urais wa shirikisho hilo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 17. Mwendwa alichaguliwa kuhudumu kwa muhula wa pili wa miaka minne baada ya kujizolea jumla ya kura 77 na kuwabwaga wapinzani wake wanne – Herbert Mwachiro, Lordvick Omondi Aduda, Boniface Osano na Dan Mule.

Mechi ya mwisho kwa Kimanzi kusimamia kambini mwa Stars ni gozi la kirafiki lililoshuhudia Kenya ikiwapepeta Zambia 2-1 uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 9.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kushuhudiwa kwenye ulingo wa soka tangu Machi baada ya serikali kusitisha shughuli zote za michezo ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

Kesi ya mauaji ya wakili Kimani yaahirishwa

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya umilisi wa lugha ya...