Michezo

Kinda watatu Wakenya wapigwa marufuku CECAFA

August 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limewapiga marufuku wachezaji watatu wa timu ya Kenya inayoshiriki katika mashindano ya kuwania ubingwa wa taji la vijana wasiozidi umri wa miaka 17, nchini Tanzania.

 Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya wachezaji hao kufanyiwa uchunguzi ambapo ilibainika wamezidi umri huo.

Mashindano hayo yalianza jana katika Uwanja wa Kitaifa jijini Dar es Salaam ambapo yatatumiwa kupata timu ya kushiriki katika fainali za kuwania ubingwa wa bara Afrika, na baadaye Kombe la Dunia.

Kufuatia hatua hiyo, kocha wa timu ya Kenya, Mike Amenga ataunda kikosi chake bila kuwajuluisha Maxwell Mulili, Lesley Otieno na AbdulMalik Hussein Abdalla.

Sheria za mashindano hayo hazikubalii timu kujaza nafasi za wachezaji waliokataliwa.

Wachezaji hao walipigwa marufuku baada ya kuchunguzwa na madaktari wa CAF, Yacine Zerquin from Algeria na Sherif Ahmed kutoka Misri.

Hatua hii imechukuliwa miaka miwili tu baada ya Kenya kupigwa marufuku kutoka fainali za wachezaji wasiozidi umrei wa miaka 20 kutokana na makossa kama hayo.

Kenya imepangiwa katika kundi moja na Uganda, Ethiopia, Djibouti na Sudan Kusini.