Michezo

Kinyago United wavuna mara mbili msimu mmoja

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

KINYAGO United iliidunga MASA bao 1-0 katika fainali na kuhifadhi taji la Top 8 wiki moja baada ya kutawazwa mabingwa wa Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14.

Kinyago United ya kocha Anthony Maina ilifanikiwa kuhimii makali ya wapinzani wao na kufuma bao hilo kipindi cha kwanza kupitia Jahson Wakachala.

”Nashukuru vijana wangu kwa kuendelea kuonyesha kazi nzuri na kuhifadhi ubingwa huo wa mechi zilizojumuisha vikosi vilivyomaliza kati ya nane bora ligini msimu wa 2018/2019,” alisema kocha wa Kinyago United na kuongeza kwamba mechi hizo huandaliwa kila mwaka ili kukuza talanta za wanasoka chipukizi mitaani.

Kinyago United chini ya nahodha, Samuel Ndonye ilitwaa tiketi ya fainali ilipogaraza Sharp Boys mabao 2-0 kupitia juhudi zake Jahson Wakachala na Geoffrey Mwangi. Kwenye nusu fainali ya pili, MASA ilisonga mbele baada ya kubeba mafanikio ya mabao 2-0 mbele ya Volcano.

Kwenye mechi za Kundi ‘A’ Kinyago United iliibuka kidedea baada ya kuvuna alama saba sawa na Volcano iliyoshindwa kwa idadi ya mabao.

Nayo Sharp Boys iliibuka wakali wa Kundi ‘B’ na kuipiku MASA maana ilikuwa imeilaza bao 1-0 licha ya kutoshana nguvu alama sita, kufunga mabao matano na kufungwa mabao mawili kila moja.

Kwenye mechi za makundi, Kinyago iliilaza Fearl mabao 3-1 kisha kuzoa magoli 3-1 dhidi ya Fernabache. Mwisho ilitoshana nguvu sare tasa na Volcano. Nayo Volcano walikomoa Fernabache magoli 5-1 kisha kubeba ufanisi wa idadi sawa na hiyo mbele ya Fearl.

Kwenye kampeni za Ligi, Kinyago United iliifadhi taji hilo kwa mara ya 12 mfululizo ilipoibuka kifua mbele kwa kuzoa pointi 57, tatu mbele ya mahasimu wao MASA.

Fernabache ambayo tangu mwanzo ilikuwa inapigiwa chapuo kubeba taji hilo ilimaliza tatu bora kwa kufikisha alama 51. Kipute cha Top Eight (nane bora) kilijumuisha Kinyago United (mabingwa watetezi), MASA, Fearl FC, Locomotive, Young Achievers, Sharp Boys, Fernabache na Volcano FC.