Kinyago United wavuruga mahasimu wao
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Kinyago United kinazidi kutetemesha katika mashindano ya soka baada ya kubeba taji la ‘Covid is the Enemy’ kwa wasiozidi umri wa miaka 14 kwenye mechi zilizopigiwa Ugani KYSD, Kinyago Village Kamukunji, Nairobi.
Kinyago ilituzwa taji hilo ilipochapa mahasimu wa tangu jadi Sharp Boys jumla ya magoli 3-2 baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 kipitia mipigo ya matuta.
Katika muda wa kawaida bao la Kinyago chini ya nahodha, Samuel Ndonye lilitupiwa kambani na Fortune Omondi naye Christopher Muthoka alisawazishia Sharp Boys.
Kwa mikwaju ya penalti Kinyago United ilipata mabao hayo kupitia Fortune Omondi, Samuel Ndonye na Abednego Wawire. Naye Christopher Muthoka alifungia Sharp Boys bao moja.
”Bila shaka nawapa hongera wachezaji wangu licha ya kupata kibarua kigumu mbele ya mahasimu wetu lakini hatimaye walifanya kweli,” kocha wa Kinyago, Anthony Maina alisema na kuongeza kuwa hata alifungana koo lake kutokana na kibarua cha kuwakosoa wachezaji wake dimbani.
”Katika mpango mzima nashukuru wachezaji wangu sana kwa kuonyesha kazi nzuri licha ya kutobeba taji hilo jinsi tulivyopania,” alisema kocha wa Sharp Boys, Boniface Kyalo na kuongeza kwamba kikosi chake kinazidi kuonyesha kuwa kina uwezo wa kukabili mahasimu hao.
Pia kocha huyo alidokeza kuwa anaamini ipo siku watakomaa mbele ya washindani wao ikiwamo Kinyago United.
PRO SOCCER ACADEMY
Nayo Pro Soccer Academy ilimaliza ya tatu baada ya kunyamazisha wenzao wa A 1000 Sportif kwa mabao 2-0 yaliyofunikwa kimiani kupitia juhudi zake Maxine Imanuel na Cliff Omengo.
Kwenye nusu fainali, Kinyago United ikibwaga A 1000 Sportif kwa magoli 3-2 yaliyopatikana kupitia Jahson Wakachala, Fortune Omondi na Michael Wandera. Nayo Sharp Boys ilijikatia tiketi ya fainali ilipozamisha Pro Soccer Academy kwa mabao 4-2 baada ya kutoshana nguvu mabao 2-2. Nao Diborn Otieno na Beca Omondi walifungia Pro Soccer Academy.
Kocha huyo wa Kinyago alipongeza wachezaji wake walionyesha kazi nzuri kwenye mashindano hayo akiwamo:Peter Gathuri, Samuel Ndonye, Jahson Wakachala, Fortune Omondi, Thierry Henry, Samuel Kamau, Michael Wandera, Abednego Wawire na Ian Ochieng.
KUKUZA
Kituo cha KYSD huandaa mashindano mengi tu ya wachezaji chipukizi kutoka mitaa ya Kinyago, Kitui Village, Shauri Moyo na Majengo kati ya maeneo mengine.
Pia KYSD inajivunia kuandaa ligi ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 14 mara 20 pia imenoa wanasoka wengi tu ambao baadhi yao tayari husakatia timu za Ligi Kuu ya KPL pia timu ya Harambee Stars kwa wasiozidi umri wa miaka 17.