• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Kipa Annette Kundu wa Harambee Starlets abanduka Lakatamia FC

Kipa Annette Kundu wa Harambee Starlets abanduka Lakatamia FC

Na CHRIS ADUNGO

KIPA wa timu ya taifa ya Harambee Starlets, Annette Kundu amepata hifadhi mpya ya soka nchini Cyprus.

Kundu kwa sasa ameingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Daraja la Kwanza nchini humo, AEL Champios kwa mkataba wa miaka miwili.

Mnamo Januari 2020, Kundu kwa pamoja na Ruth Ingotsi ambaye ni beki wa Starlets, walijiunga na kikosi cha Lakatamia FC cha Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Cyprus kwa mkataba wa miaka mitatu.

AEL Champions walitua kileleni mwa jedwali la vikosi tisa vya Ligi ya Daraja la Kwanza msimu huu wa 2020-21 baada kukamilisha mechi za raundi ya kwanza.

Kwa kipindi kifupi alichochezea Lakatamia FC, Kundu aliwajibishwa katika mechi 12 na akafungwa jumla ya mabao 16 kabla ya msimu wa 2019-20 katika soka ya Cyprus kusitishwa kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19.

“Ni fahari tele kwa mwanasoka yeyote kupata fursa mpya ya kukabiliana na changamoto za kila sampuli. Napania kujitahidi zaidi kwa matumaini kwamba kujituma kwangu kutaendelea kunipa fursa ya kuvalia jezi za timu ya taifa ya Starlets,” akasema Kundu.
Kwa mujibu wa kampuni ya Soccer Expo inayomwakilisha Kundu, hatua ya mwanasoka huyo kujiunga na AEL ni fursa nzuri kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 kujikuza zaidi kitaaluma.

“Hii ni mojawapo ya dili za kiwango cha juu zaidi kwa mwanasoka wa haiba ya Kundu kutia saini. Kwa kuingia katika sajili ya AEL, sasa yuko pazuri zaidi kushiriki soka ya Klabu Bigwa Ulaya (UEFA) katika siku za hivi karibuni,” ikasema sehemu ya taarifa ya Soccer Expo.

Tangu 2014, Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Cyprus ndiyo imesalia kuwa ya pekee kwa soka wanawake katika taifa hilo, kumaanisha kwamba hakuna timu za kushuka ngazi wala kupanda daraja mwishoni mwa kila msimu.

Kundu na Ingotsi ni miongoni mwa wanasoka matata wa Starlets ambao wanajivunia kusakata soka ya kulipwa katika mataifa ya ughaibuni baada ya kupata dili za nguvu katika kipindi cha miezi michache iliyopita.

Wengine ni Cynthia Shilwatso aliyejiunga na EDF Logrono ya Uhispania kwa mkataba wa miaka mitatu na Lily Awuor anayejezea Borussia Pankow ya Ujerumani.

Huku vikosi vya Kenya vikikabiliwa na panda-shuka tele za kifedha, fursa za kutandaza soka ya kulipwa katika mataifa ya majuu ni jukwaa zuri kwa vipusa wa Starlets kujiendeleza kitaaluma na kiuchumi.

Kundu na Ingotsi walikuwa sehemu ya kikosi cha Starlets kilichonyanyua ubingwa wa Cecafa Senior Challenge mwaka jana baada ya kuwapiga wenyeji na mabingwa mara mbili, Tanzania 2-0 kwenye fainali iliyochezewa jijini Dar es Salaam.

Kundu hakufungwa bao lolote katika kivumbi hicho na akatawazwa Kipa Bora wa Cecafa Senior Challenge.

  • Tags

You can share this post!

Vihiga United waingiwa na hofu wanapojiandaa kwa mchujo

Mwamba RFC kukosa uwanja wa nyumbani