• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 7:55 AM
Kipa Henderson kuwadakia Man-United hadi Juni 2025

Kipa Henderson kuwadakia Man-United hadi Juni 2025

Na CHRIS ADUNGO

KIPA Dean Henderson wa Manchester United ametia saini mkataba mpya utakaomdumisha kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi Juni 2025.

Henderson, 23, alivalia jezi za Sheffield United kwa mkopo katika kipindi cha misimu miwili iliyopita. Anapigiwa upatu wa kumpiku sasa David De Gea uwanjani Old Trafford na kuwa mlinda-lango chaguo la kwanza.

Mnamo Agosti 25, Henderson alijumuishwa na kocha Gareth Southgate katika kikosi cha wanasoka atakaowategemea katika mechi zijazo za Uefa Nations League dhidi ya Iceland na Denmark.

“Imani ambayo kocha na vinara wa klabu wamenionyesha kupitia mkataba huu ni kubwa sana. Sasa itanilazimu kujituma zaidi na kufikia matarajio makubwa ambayo kila mmoja anatazamia kutoka kwangu,” akasema mlinda-lango huyo.

Akivalia jezi za Sheffield United, Henderson alichezea kikosi hicho jumla ya mechi 86 tangu ajiunge nacho mnamo 2018 na akakisaidia katika msimu wake wa kwanza, kupanda daraja hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).Katika kampeni za EPL msimu huu wa 2019-20, Sheffield United walikamilisha kampeni zao katika nafasi ya tisa huku wakimtegemea sana Henderson aliyekuwa kipa wao chaguo la kwanza.

Henderson ambaye ana fursa ya kurefusha mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi ugani Old Trafford, amekuwa mchezaji wa Man-United tangu akiwa mtoto wa umri wa miaka 14 pekee na aliitwa kambini mwa timu ya taifa ya Uingereza kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2019.

“Ni furaha kubwa kwamba Henderson ametia saini mkataba mpya. Alijivunia misimu miwili ya kuridhisha zaidi kambini mwa Sheffield United ambao walimwajibisha mara kwa mara. Kwa sasa ana tajriba ya kutosha na mchezo wake umeimarika pakubwa,” akasema kocha Ole Gunnar Solskjaer.

  • Tags

You can share this post!

Aubameyang yuko karibu kutia saini mkataba mpya Arsenal

Kiungo Gareth Barry astaafu soka akiwa na umri wa miaka 39