Michezo

Kipa Mendy ang'aa licha ya Chelsea kula sare ya Sevilla kwenye UEFA ugani Stamford Bridge

October 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

KIPA Edouard Mendy kwa sasa ana kila sababu ya kuwa mlinda-lango chaguo la kwanza la Chelsea na kumweka Kepa Arrizabalaga kwenye ulazima wa kusugua benchi.

Hii ni baada ya nyani huyo raia wa Senegal kupangua makombora mengi ya Sevilla na kusaidia waajiri wake kuambulia sare tasa dhidi ya mabingwa hao wa Europa League kwenye UEFA mnamo Oktoba 20.

Sare hiyo iliyosajiliwa na masogora wa kocha Frank Lampard bado ni nafuu zaidi ikizingatiwa kwamba Krasnodar ya Urusi pia walilazimishia Rennes ya Ufaransa sare ya 1-1 ugenini kwenye mechi nyingine ya Kundi E.

Chelsea walimsajili Mendy, 28, kutoka Rennes kwa mkataba wa miaka mitano mnamo Septemba baada ya kuwajibishwa katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mara 25 katika msimu wa 2019-20.

Matokeo duni ya Kepa ambaye ni raia wa Uhispania katika mechi muhimu ni kiini cha kocha Lampard kumtema katika kikosi cha kwanza cha Chelsea msimu uliopita. Mojawapo ya mechi hizo ni ile ya fainali ya nusu-fainali ya Kombe la FA iliyoshuhudia nafasi ya Kepa, 25, ikitwaliwa na kipa mkongwe, Willy Caballero, 38.

Kati ya sajili wapya waliogharimu Chelsea zaidi ya Sh35 bilioni muhula huu, ni Mendy, Ben Chilwell na Thiago Silva ndio walioridhisha zaidi kambini mwa kikosi hicho ambacho kwa sasa kinajiandaa na Manchester United kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Old Trafford Jumamosi hii.

Sevilla waliopiga Wolves na Manchester United kwenye robo-fainali na nusu-fainali kabla ya kuwalaza Inter Milan kwenye fainali ya Europa League msimu jana, walikosa kutumia vyema nafasi chache za wazi walizozipata dhidi ya Chelsea. Mchuano huo ulikuwa wa tano kati ya nane kwa Chelsea kuambulia sare kwenye UEFA ugani Stamford Bridge.

Huku Sevilla wakiendeleza rekodi ya kutoshindwa kwenye mechi tano zilizopita za UEFA, Chelsea wameshinda mchuano mmoja pekee wa UEFA kati ya 10 iliyopita dhidi ya mpinzani kutoka Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).