Kipa wa Misri mwenye miaka 45 aweka historia
Na GEOFFREY ANENE
Ni rasmi kipa wa Misri, Essam El-Hadary ni mchezaji mzee kuwahi kushiriki Kombe la Dunia baada ya kuanzishwa na Mafirauni dhidi ya Saudi Arabia katika mechi ya mwisho ya Kundi A mjini Volgograd nchini Urusi, Jumatatu.
Kocha Mkuu wa Misri, Hector Cuper amejumuisha jagina huyu katika rodha ya wachezaji 11 wa kwanza wanaokabiliana na Saudi Arabia saa kumi na moja saa ya Kenya.
El-Hadary alikuwa kwenye benchi dhidi ya wenyeji Urusi na mabingwa wa zamani Uruguay katika mechi ambazo timu yake ilipoteza 3-1 na 1-0 mtawalia, huku Mohamed El-Shennawy, 29, akianza michumani katika mechi hizo.
Kipa huyu mwenye umri wa miaka 45 amefuta rekodi ya kipa Faryd Mondragon, ambaye alichezea Colombia dhidi ya Japan katika makala yaliyopita nchini Brazil mwaka 2014 akiwa na umri wa miaka 43 na siku tatu.
Misri inapiga mechi yake ya mwisho kabla ya kufunga virago baada ya kupoteza mechi zake mbili za kwanza.
Wamisri walikuwa wanarejea katika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990.
Macho yote pia yatakuwa kwa mvamizi matata kutoka Misri, Mohamed Salah, ambaye ni mchezaji bora wa Afrika mwaka 2017 na nchini Uingereza msimu 2017-2018. Aling’aa sana akiwakilisha mabingwa mara 18 wa Uingereza, Liverpool, katika Ligi Kuu na Klabu Bingwa Ulaya.