• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Kipa wa zamani wa Chelsea afariki

Kipa wa zamani wa Chelsea afariki

Na CHRIS ADUNGO

KIPA wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Uingereza, Peter ‘The Cat’ Bonetti ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 78 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chelsea, Bonetti alikuwa kati ya makipa waliotamba pakubwa katika miaka ya 60 na 70 na miongoni mwa wachezaji wao bora zaidi wa muda wote.

Japo alikuwa sehemu ya kikosi cha Uingereza kilichonyakua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 1966, Bonetti hakuwajibishwa katika mchuano wowote katika gozi hilo.

Alichezeshwa mara saba na timu ya taifa ya Uingereza katika Kombe la Dunia mnamo 1970 kabla ya kikosi chao kubanduliwa na Ujerumani katika hatua ya robo-fainali.

Zaidi ya kuvalia jezi za Chelsea waliojivunia maarifa yake katika jumla ya mechi 729, Bonetti aliwahi pia kupiga soka ya kulipwa nchini Amerika kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 katika vikosi vya St Louis Stars, Dundee United na Woking FC.

Kufikia sasa, ni aliyekuwa nahodha wa Chelsea, Ron Haris ndiye anayejivunia rekodi ya kuwajibikia kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara nyingi zaidi. Kwa upande wake, Bonetti aliwahi kushikilia rekodi ya kipa ambaye hakufungwa bao lolote katika mechi nyingi zaidi kambini mwa Chelsea hadi 2014 ambapo rekodi hiyo ilivunjwa na Petr Cech.

Alikuwa tegemeo kubwa katika ushindi uliovunwa na Chelsea dhidi ya Leeds United katika fainali ya Kombe la FA mnamo 1970.

Aliwahi pia kunyanyulia Chelsea ubingwa wa League Cup mnamo 1965 na taji la Uefa Cup Winners’ Cup mnamo 1971.

Bonetti aliwahi pia kuibuka wa pili katika tuzo ya kuwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka mnamo 1969-70.

Baada ya kuangika daluga zake, Bonetti alijitosa katika ulingo wa ukufunzi na akawa kocha wa makipa kambini mwa Chelsea, Uingereza, Manchester City, Newcastle United na Fulham.

Mbali na Greg Clarke ambaye ni mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA), wanasoka wengine ambao wamemwomboleza Bonetti ni Peter Shilton anayeshikilia rekodi ya kuchezea Uingereza idadi kubwa zaidi ya michuano ya kimataifa na nahodha wa zamani wa Chelsea, John Terry.

  • Tags

You can share this post!

Wakristo sasa wafanya ibada milimani na mapangoni kisiri

Wabunge wazee kufungiwa nje ya vikao

adminleo