Kipchoge aongeza Sydney Marathon katika mbio atakazotimka mwaka huu
MFALME wa zamani wa mbio za kilomita 42 za Olimpiki, Eliud Kipchoge ametangaza kuwa marathon yake ya pili atakayoshiriki mwaka huu itakuwa jijini Sydney, Australia, hapo Agosti 31.
Kipchoge,40, anajiandaa kushiriki London Marathon nchini Uingereza hapo Aprili 27.
Mbio hizo mbili za kilomita 42 ni sehemu ya ligi ya Marathon Kuu Duniani (WMM) mwaka huu zinazojumuisha Tokyo Marathon (Machi 2), Boston Marathon (Aprili 21), London Marathon (Aprili 27), Sydney Marathon (Agosti 31), Berlin Marathon (Septemba 21), Chicago Marathon (Oktoba 12) na New York Marathon (Novemba 2). Sydney imejumuishwa katika ligi hiyo ya kifahari kwa mara ya kwanza kabisa.
Kipchoge ameshinda mbio 11 katika ligi hiyo tangu ajitose mitimko ya marathon mwaka 2013. Ripoti zinasema kuwa Sydney Marathon ilijaribu kumshawishi ashiriki makala ya 2023 na tena 2024, lakini haikufaulu.

“Kukamilisha mbio za 42km chini ya saa mbili kunamweka Eliud Kipchoge katika orodha ya masupastaa wakongwe kama Roger Bannister, Usain Bolt, Muhammad Ali, Roger Federer na Dawn Fraser. Tunasubiri kumkaribisha,” rais wa Shirikisho la Riadha la Australia, Jane Fleming, amenukuliwa akisema.
Naye Kipchoge katika taarifa kwa vyombo vya habari amesema kuwa anasubiri kwa hamu kubwa kutimka nchini Australia, japo amekiri kila marathon ni changomoto mpya na yuko tayari kupima uwezo wake katika barabara za Sydney.
“Ukimbiaji una kipaji cha kuunganisha watu. Ninasubiri kuungana na jamii ya wakimbiaji nchini Australia wakati huu taifa hilo na ulimwengu kwa jumla unakumbatia mchezo huo unaokuwa kwa haraka”
Kipchoge ni mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia ya 42km ya saa 2:01:09 aliyoweka mjini Berlin, Ujerumani mwaka 2022. Kelvin Kiptum alifuta rekodi hiyo akishinda Chicago Marathon mwaka 2023 kwa 2:00:35.
Katika marathon yake ya kwanza tangu akose kukamilisha 42km kwenye Michezo ya Olimpiki mjini Paris nchini Ufaransa mwaka jana, Kipchoge atatimka London Marathon ambapo atawania taji dhidi ya bingwa mtetezi Alex Mutiso pamoja na Sabastian Sawe, Timothy Kiplagat, Hillary Kipkoech, Waethiopia Tamirat Tola, Kenenisa Bekele na Milkesa Mengesha, Mganda Jacob Kiplimo na Mholanzi Abdi Nageeye, miongoni mwa wengine.