KIPENGA: Udhaifu wa Mourinho ni kukosa uvumilivu unaofaa
Na JOB MOKAYA
Msimu umekamilika huku Jose Mourinho akiambulia nunge kama mwenzake wa Arsenal, Arsene Wenger.
Chelsea, ingawa haikufuzu kucheza UEFA Champions League, angalau ilinyakua Kombe la FA baada ya kuishinda Manchester United bao moja kwa bila.
Kwenye mechi hiyo ya FA, Anthony Martial aliingia zikiwa zimesalia dakika chache tu mpira kukamilika. Hata hivyo, ujio wake haukusaidia kitu kwani vijana wa Antonio Conte walihami kwa maarifa yote bao lao moja lililofungwa na Eden Hazard kwa mkwaju wa penalti.
Ilivyo sasa, itabidi wachezaji kadhaa waondoke Old Trafford na kutafuta huduma kwingineko. Miongoni mwa wachezaji hao ni Anthony Martial.
Huenda Martial ndiye mchezaji anayependwa sana na mashabiki wengi wa Old Traford. Hata hivyo, kupendwa na mashabiki si sawa na kupendwa na kocha.
Martial hapendwi na Mourinho. Sio kwamba Martial hajui mpira.
La hasha. Tatizo la Martial ni kwamba anahitaji muda mwingi ili kuwa mchezaji bora. Anahitaji kucheza mechi nyingi ili kuimarisha mchezo wake. Anahitaji uvumilivu mwingi ili kupata makali.
Tatizo ni kwamba muda huo, mechi hizo, uvumilivu huo hanao Mourinho. Mourinho anapopewa nafasi ya kufunza timu, huwa kuna matarajio mengi sana kwake. Kwamba lazima ashinde mataji muhimu.
Hivyo, Mourinho hana muda wa kuwapa wachezaji nafasi nyingi za kucheza ili wajiimarishe. Muda wake mchache ni wa kushinda mechi na kunyakua vikombe.
Mourihno hana uvumilivu mwingi na wachezaji wanaojaribu kujitambua. Vyombo vya habari pia havina uvumilivu na Mourihno. Wamiliki pia hawana uvumilivu na Mourinho.
Kutokana na mchezo wa Martial kuwa duni kiasi hiki, Mourinho ameondoa imani kwake.
Na kutomwekea huko imani kulikomfanya Martial kuachwa nje ya kikosi cha Ufaransa juma lililopita.
Ubaya pekee wa Martial ni kujipata ndani ya timu ya Mourinho. Mourinho ni kocha wa kuchezesha mpira wa kujihami. Mashambulizi yake mengi yanatoka nyuma kuelekea mbele.
Martial ataifaa Liverpool
Hivyo hata mastraika wake wanacheza kutoka nyuma kuelekea mbele.Huo ndio ubaya wa Martial. Martial ataimarika sana akijipata kwenye timu za kushambulia. Timu kama vile Liverpool.
Timu kama vile Manchester City. Timu kama vile Arsenal. Timu kama vile Tottenham. Labda timu kama vile Chelsea.
Basi Martial afanyaje? Hayuko Liverpool, hayuko Manchester City, hayuko Arsenal, hayuko Tottenham. Hayuko Chelsea. Afanye nini?
Jibu ni rahisi sana. Itabidi Martial aondoke Manchester United na kutafuta timu itakayomvumilia na pia kuthamini mchezo wake. Anaweza kujiunga na timu za England au hata kuelekea Bundesliga Ujerumani, La Liga Uhispania au hata League 1 Ufaransa.
Kwa Mourinho, si bora kumuuza Martial. Bora ni kumtuma nje kwa mkopo ili apate mechi nyingi za kujiimarisha.
Na asimuuze kwa timu kama Barcelona au Real Madrid. La, huko yatampata ya Manchester United.
Amuuze (kwa mkopo) kwa timu nzuri ila si bora kama vile Borussia Dortmund ya Ujerumani, Atletico Madrid ya Uhispania au Marseille FC ya Ufaransa ama timu nyingine kama hizo.