Michezo

Kipruto aongoza kwa kasi mbio za kilomita 10 mwaka huu

April 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Rhonex Kipruto anashikilia kasi ya juu ya mbio za kilomita 10 mwaka 2018 na pia kuwahi kushuhudiwa nchini Marekani baada ya kushinda taji la UAE Healthy Kidney 10K mjini New York City kwa dakika 27:08 Jumapili.

Chipukizi huyu mwenye umri wa miaka 18 alifuta rekodi ya kasi ya juu kuwahi kuwekwa na raia wa kigeni nchini Marekani ya dakika 27:11 ya Mkenya Sammy Kipketer iliyokuwa imedumu tangu mwaka 2002. Kipketer aliiweka mjini New Orleans.

Kipruto alivunja rekodi ya UAE Healthy Kidney 10K ya dakika 27:35, ambayo Mkenya Leonard Patrick Komon aliweka mwaka 2011.

Muda wa Kipruto unaongoza jedwali la kasi ya juu mwaka 2018. Alifuta ule uliokuwepo wa dakika 27:26 uliowekwa na Mkenya Emmanuel Kiprono mjini Paderborn nchini Ujerumani mnamo Machi 31, 2018.

Kasi ya Kipruto ni ya saba bora duniani katika sehemu ya mashindano inayokubalika na Shirikisho la Riadha duniani (IAAF).

Kipruto alikamilisha umbali huo sekunde 11 mbele ya Mkenya mwenzake Mathew Kimeli (27:19) naye Muethiopia Teshome Mekonen akafunga tatu-bora (28:10).

Waethiopia Buze Diriba (32:04) na Aselefech Mergia (32:06) walifagia nafasi mbili za kwanza katika kitengo cha wanawake, huku Mkenya Monicah Ngige akiridhika na nafasi ya tatu (32:15).

Rekodi za dunia za mbio za kilomita 10 zinashikiliwa na Wakenya Joyciline Jepkosgei (29:43) na Komon (26:44). Jepkosgei aliweka rekodi hiyo katika mbio za mseto mjini Prague katika Jamhuri ya Czech mnamo Aprili 1 mwaka 2017 naye Komon alitimka kasi hiyo mjini Utrecht nchini Uholanzi mwaka 2010. Rekodi ya wanawake pekee ya mbio za kilomita 10 ya dakika 30:29 inashikiliwa na Mmroko Asmae Leghzaoui tangu mwaka 2002.