Kipruto ashindia Kenya shaba, Kipchoge akiuma nje katika marathon Olimpiki
BINGWA wa Tokyo Marathon Benson Kipruto alishindia Kenya medali ya shaba katika mbio za masafa marefu za Michezo ya Olimpiki mjini Paris nchini Ufaransa mnamo Jumamosi, Agosti 10, 2024.
Kipruto, ambaye kabla ya mbio hizo za kilomita 42 alitangaza kuwa atakimbia kwa heshima ya mshikilizi wa rekodi ya dunia Kelvin Kiptum aliyeaga dunia katika ajali ya barabarani mwezi Februari mwaka huu, alikamilisha mbio kwa saa 2:07:00.
Bingwa wa 2016 na 2021 Eliud Kipchoge aliyekuwa akifukuzia kutetea taji na kuwa mtimkaji wa kwanza kabisa mwanamume kutawala marathon mara tatu mfululizo kwenye Olimpiki aliambulia patupu.
Kipchoge hakuwahi kuingia katika orodha ya wakimbiaji 50 – bora katika shindano hilo la marathon nchini Ufaransa mnamo Jumamosi.
Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 39 aliishia kukosa kumaliza mbio baada ya kuaminika kujiuzulu baada ya karibu kilomita ya 30.
Ni matokeo mabaya kabisa amewahi kupata baada ya kuwa nambari 10 kwenye Tokyo Marathon mwezi Machi 2024.
Muethiopia Tamirat Tola aliibuka mshindi kwa rekodi mpya ya Olimpiki saa 2:06:26 baada ya kufuta rekodi ya mwendazake Samuel Wanjiru 2:06:32 iliyodumu tangu 2008.
Tola hakuwapa wapinzani wake nafasi baada ya kuchukua uongozi kabisa katika kilomita 21 za mwisho.
Ukakamavu wake ulishindia taifa lake medali ya dhahabu ya kwanza katika makala haya ya 33 na pia ya kwanza ya marathon tangu mwaka 2000.
Mbelgiji Bashir Abdi aliyepata nishani ya shaba mjini Tokyo nchini Japan mwaka 2021, aliridhika na ile ya fedha kwa 2:06:47.
Kipruto, 33, ni mwanamume wa saba kutoka Kenya kupata medali kwenye Olimpiki baada ya Douglas Wakiihuri (fedha mwaka 1988), Erick Wainaina (shaba 1996 na fedha 2000), Wanjiru (dhahabu 2008), Abel Kirui (fedha 2012), Wilson Kipsang (shaba 2012) na Eliud Kipchoge (dhahabu 2016 na 2020).
Alexander Mutiso aliyepigiwa upatu kufanya vyema baada ya kushinda London Marathon mwezi Aprili 2024, alikamata nafasi ya 21 kwa 2:10:31.
Kenya sasa imezoa medali saba kupitia kwa Beatrice Chebet (dhahabu ya 5,000m na 10,000m), Faith Kipyegon (fedha ya 5,000m), Mary Moraa (800m), Faith Cherotich (3,000m kuruka viunzi na maji) na Abraham Kibiwot (3,000m kuruka viunzi na maji) na Kipruto (shaba ya marathon).
Bingwa wa dunia Victor Kiplangat (Uganda) na Kenenisa Bekele (Ethiopia) walimaliza katika nafasi ya 37 na 39, mtawalia.