• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Kipruto na Cherono waahidi makuu katika Valencia Marathon

Kipruto na Cherono waahidi makuu katika Valencia Marathon

Na CHRIS ADUNGO

MSHINDI wa nishani ya shaba katika marathon ya dunia mnamo 2019, Amos Kipruto amesema kwamba analenga kuimarisha matokeo yake kwa kusajili muda bora zaidi kwenye makala yajayo ya mbio za Valencia Marathon.

Kipruto atapania kutumia mbio hizo za Valencia mnamo Disemba 6 nchini Uhispania kuimarisha muda wake bora wa saa 2:05.43 aliosajili kwenye Amsterdam Marathon mnamo 2018.

Mwanaridha huyo amekuwa akishiriki mazoezi ya kina katika eneo la Kapsabet, Kaunti ya Nandi kwa miezi kadhaa saa tangu alipoambulia nafasi ya 18 kwenye mbio za Tokyo Marathon mnamo Machi 2020 baada ya kusajili muda wa saa 2:08:00.

“Umekuwa mwaka wenye panda-shuka tele na msimu huu wangu ulianza kwa mbio za Tokyo Marathon. Nilikuwa na jeraha la mguu wakati huo. Sasa niko katika hali shwari na mashabiki wana kila sababu ya kutarajia makuu kutoka kwangu,” akasema Kipruto huku akionya kwamba idadi kubwa ya Waethiopia kwenye mbio hizo itakuwa kiini cha ushindani mkali zaidi kushuhudiwa na uwezekano wa rekodi mpya kuwekwa.

Japo itakuwa mara yake ya kwanza kushiriki Valencia Marathon, atapania kujinyanyua baada ya kuambulia nafasi ya 18 kwenye mbio za Tokyo Marathon mnamo Machi.

Kipruto aliyeibuka wa tatu katika Tokyo Marathon mnamo 2019 (2:06.33), alipata umaarufu zaidi 2018 alipokamilisha Berlin Marathon katika nafasi ya pili nyuma ya Eliud Kipchoge aliyeweka rekodi ya dunia ya saa 2:01:39 katika mbio hizo.

Mshindi wa mbio za Boston na Chicago Marathon, Lawrence Cherono ataongoza kikosi cha Kenya kwa upande wa wanaume jijini Valencia. Kinde Atanaw aliyeweka rekodi ya saa 2:03:51 mnamo 2019, atalenga kuhifadhi ufalme wake japo atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Mwethiopia mwenzake, Birhanu Legese ambaye anajivunia muda wa tatu wa kasi zaidi katika mbio za mita 42 (2:02:48).

Katika miaka ya hivi karibuni, jiji la Valencia nchini Uhispania limekuwa jukwaa maridhawa kwa wanariadha kuvunja baadhi ya rekodi kwenye mbio za masafa marefu.

Muda bora na wa kasi zaidi huenda ukashuhudiwa kwenye mbio za kilomita 42 ambazo zimevutia wanariadha wa haiba kubwa akiwemo bingwa wa Tokyo Marathon mnamo 2019, Ruti Aga (2:18:34) atakayetoana jasho na Mwethiopia mwenzake Birhane Dibaba (2:18:35).

Mare Dibaba, aliyeibuka bingwa wa dunia katika marathon mnamo 2015 pia atanogesha kivumbi cha Valencia Marathon kwa pamoja na Waethiopia Zeineba Yimer na Tigist Girma wanaojivunia muda wa chini ya saa 2:20. Jordan Hasay wa Amerika na mshikilizi wa rekodi ya Nusu Marathon, Mkenya Peres Jepchirchir pia watakuwa sehemu ya washiriki wa mbio hizo kwa upande wa wanawake.

Wanariadha wengine ambao wamethibitisha kushiriki mbio hizo za Valencia Marathon ni bingwa wa zamani wa dunia Lelisa Desisa, mshikilizi wa rekodi ya bara Ulaya Kaan Kigen Ozbilen na mshikilizi wa rekodi ya mbio za kilomita 21 nchini Ethiopia, Jemal Yimer. Itakuwa mara ya kwanza kwa Yimer kunogesha mbio za kilomita 42.

  • Tags

You can share this post!

DARAJA LA MUNGU: Daraja la maumbile ya kiasili linalookoa...

DPP kuwasilisha mashahidi 30 kwa kesi ya Jumwa