• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
Kipsang atangaza kupigania ubingwa London Marathon

Kipsang atangaza kupigania ubingwa London Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa zamani wa rekodi ya dunia ya mbio za wanaume za kilomita 42, Wilson Kipsang’ ametangaza Januari 16 atarejea kuwania taji la London Marathon nchini Uingereza hapo Aprili 28, 2019.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Mkenya huyu, ambaye anajivunia mataji la London Marathon mwaka 2012 na 2014, amesema yuko tayari kushindania taji dhidi ya mfalme wa mbio hizi mwaka 2015, 2016 na 2018 Eliud Kipchoge, ambaye anashikilia rekodi ya dunia na London Marathon.

“Nafurahia kutangazia ulimwengu kwamba nitashiriki mbio za London Marathon (mwaka 2019). Baada ya kukosa makala mawili yaliyopita, nitakuwa tayari kutimka katika barabara za London tena,” alisema Kipsang’, ambaye ameambia tovuti ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwamba “Niko makini kutwaa taji.”

Kitakuwa kivumbi kikali kwa sababu mbali na Kipchoge, ambaye anajivunia rekodi ya saa 2:01:39 katika mbio za kilomita 42, pia kuna Muethiopia Shura Kitata na Muingereza Mo Farah waliomaliza makala yaliyopita katika nafasi ya pili na tatu, mtawalia.

Mwaka 2018, Kipchoge alijizolea tuzo ya Sh5,594,600 kwa ushindi wake na kuongezwa bonasi ya Sh10,172,000 kwa kukata utepe chini ya saa 2:05:00. Alinyakua taji kwa saa 2:04:17. Tuzo ya Sh2,543,000 ilitengewa kwa mkimbiaji atakayevunja rekodi ya London Marathon ya wanaume ya saa 2:03:05 ambayo Kipchoge aliweka mwaka 2016, lakini hakuna aliyefanikiwa kuifuta. Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Abraham Kiptum (dakika 58:18) pia atashiriki.

Malkia wa Chicago Marathon, Brigid Kosgei ameongezwa katika orodha ya kinadada watakaowania taji hili la kifahari.

Kosgei alikamilisha London Marathon mwaka 2018 katika nafasi ya pili nyuma ya Mkenya mwenzake Vivian Cheruiyot kabla ya kujishindia taji la Chicago miezi sita baadaye.

You can share this post!

SHAMBULIO: Serikali itagharamia matibabu ya waathiriwa wote...

Ingwe wajinyanyua KPL

adminleo