• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
Kiptum ajishindia mamilioni Hong Kong Marathon

Kiptum ajishindia mamilioni Hong Kong Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Barnabas Kiptum alijizolea tuzo ya mshindi ya Sh6,510,400 na kuongezwa bonasi ya Sh1,001,600 baada ya kutwaa taji la mbio za Standard Chartered Hong Kong Marathon kwa rekodi mpya ya saa 2:09:20 mnamo Februari 17, 2019.

Kiptum, ambaye alipokea Sh1,502,400 kwa kumaliza Hong Kong Marathon katika nafasi ya tatu mwaka 2018, alitawala mbio hizi za kilomita 42 kutoka mwanzo hadi utepeni. Alifuta rekodi ya Muethiopia Melaku Belachew ya 2:10:31 iliyowekwa mwaka 2017.

Nafasi za pili na tatu, ambazo zinaandamana na tuzo ya Sh3,004,800 na Sh1,502,400 ziliwaendea Waethiopia Wolde Dawit (2:11:11) na Tadese Getachew (2:11:12). Mkenya Joel Kimurer Kemboi (2:11:13) alitia mfukoni Sh1,001,600 kwa kumaliza katika nafasi ya nne.

Raia wa Belarus, Volha Mazuronak alipokea zawadi sawa na Kiptum baada ya kunyakua taji la kinadada kwa rekodi mpya ya Hong Marathon ya saa 2:26:13.

Alivunja rekodi ya Muethiopia Gulume Tollesa aliyeshinda makala ya mwaka 2018 kwa saa 2:29:37. Mbahraini Eunice Chumba (2:30:02) na Muethiopia Jemila Wortesa (2:32:06) walifunga mduara wa tatu-bora katika kitengo cha kinadada. Wakimbiaji 74, 000 walishiriki makala ya mwaka huu.

  • Tags

You can share this post!

Oliech akosa nafasi kwa kikosi cha AFCON na CHAN

Cecafa yatangaza ratiba ya mechi za 2019

adminleo