Kiptum alifariki kutokana na majeraha ya kichwa – Upasuaji
NA TITUS OMINDE
KWA muda wa saa tano, mwanapatholojia wa serikali Johansen Oduor amekuwa makini akifanya uchunguzi wa kina kwa mwili wa marehemu mshikilizi wa rekodi ya mbio za Marathon Kelvin Kiptum katika hospitali ya Eldoret mnamo Jumatano.
Dkt Oduor alithibitisha muda mfupi baadaye kuwa Kiptum alifariki kutokana na majeraha mengi kichwani kufuatia ajali ambayo alipata akiendesha gari lake katika barabara ya Eldoret-Eldama Ravine mnamo usiku wa Februari 11 kuamkia Februari 12, 2024.
Mpasuaji mkuu wa serikali aidha amefichua staa huyo wa Marathon aliaga dunia kutokana na majeraha mabaya ya kichwa ambayo pia yalisababisha kuvunjika kwa fuvu la kichwa.
Isitoshe, Kiptum pia alianguka kwa kishindo ambapo mbavu zake zilivunjika.
Dkt Oduor alisema kutokana na uvumi ulioenezwa kuhusu chanzo cha kifo cha mwanariadha huyo, alilazimika kufika Eldoret kufanya upasuaji wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo hicho ili kuepusha uvumi zaidi.
“Wakati wa kufanya uchunguzi huo, matokeo yalikuwa hivi, marehemu Kelvin alikuwa na majeraha makubwa kichwani, kuvunjika kwa fuvu la kichwa, uti wa mgongo ulikuwa umetokeza kwenye fuvu kwa sababu ya kuvunjika,” alisema Dkt Oduor
Dkt Oduor aliendelea kufichua kuwa kulikuwa na mivunjiko zaidi katika pande zote mbili za mbavu pamoja na baadhi ya majeraha ya mapafu kutokana na athari za ajali hiyo.
“Zaidi ya hayo kulikuwa na mivunjiko kwa pande zote mbili za mbavu, upande wa kushoto ubavu wa kwanza na wa pili ulikuwa umevunjika pamoja na ubavu wa kwanza,pili, tatu, nne na wa tano zote zilivunjika,” alisema Dkt Oduor.
Vile vile Dkt Oduor alifichua kuwa marehemu alikuwa na majeraha kadhaa kwenye mapafu.
Wakati uo huo Dkt Oduor alifichua kuwa sampuli zaidi zimepelekwa Nairobi kwa uchunguzi zaidi ikizingatiwa kuwa uchunguzi zaidi unafanywa kubaini chanzo cha kifo hicho.
“Tumechukua sampuli zaidi kwa uchunguzi zaidi kwa sababu kifo hiki kilizua hisia mbalimbali nnchini ambapo makachero bado wanendelea na uchunguzi zaidi,” aliongeza Dkt Oduor.
Msemaji wa familia ya Kiptum, Bw Philip Kiplagat ambaye alishuhudia uchunguzi huo wa maiti, alisema kuwa familia hiyo iliridhishwa na ripoti ya uchunguzi wa maiti iliyotolewa mwanapatholojia wa serikali.
Bw Kiplagat hata hivyo, alisema familia hiyo inasubiri kwa hamu uchambuzi zaidi wa sampuli zilizotumwa Nairobi jinsi Dkt Oduor alivyoripoti.
“Kama familia tumeridhishwa na ripoti ya uchunguzi wa maiti na jinsi ambavyo Dkt Oduor amesema, uchunguzi zaidi bado unaendelea na ndio maana tunasubiri kwa hamu matokeo zaidi kutoka kwa sampuli zilizopelekwa Nairobi,” alisema Bw Kiplagat.
Marehemu atazikwa katika eneo la Naiberi katika Kaunti ya Uasin Gishu.
Familia ya marehemu inajengewa nyumba aushi kufuatia amri ya Rais William Ruto.