Kipyegon anaswa kwa kutumia dawa za kusisimua misuli
NEHEMIAH Kipyegon atakuwa shabiki wa riadha baada ya kupigwa marufuku miaka mitatu na Kitengo cha Maadili cha Shirikisho la Riadha Duniani (AIU) kwa kututumua misuli.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi, AIU imesema kuwa Kipyegon alipatikana na kosa la kutumia dawa ya aina ya Trimetazidine ambayo iko katika orodha ya dawa Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya Duniani (WADA) limekataza wanamichezo hawafai kutumia.
Kipyegon alikamata nafasi ya pili kwenye mbio za Lagos Marathon nchini Nigeria mwezi Februari na kuwa nambari tatu Massif Forestier Half Marathon mjini Nuaille, Ufaransa mwezi Machi.
Amepoteza matokeo hayo pamoja na pointi na zawadi zozote alipata kutoka kwa mashindano yote kuanzia Lagos Marathon 2025 hadi sasa.
Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 27 anaingia katika orodha ndefu ya wanamichezo 132 kutoka Kenya wanaotumikia marufuku kwa kukiuka sheria zinazowakataza kutumia dawa za kusisimua misuli.