Michezo

Kirenge kusalia KPL

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya Piscas Kirenge kukatiza rasmi uhusiano wake na Wazito FC, fowadi huyo mzawa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hana nia yoyote ya kuagana na soka ya Ligi Kuu ya Kenya hivi karibuni.

Akifichua maazimio yake, Kirenge amesisitiza kwamba anapania kusalia humu nchini kunogesha kampeni za KPL akiwa mchezaji wa kikosi kingine kwa kipindi cha misimu miwili ijayo kabla ya kurejea nyumbani kwao.

Kirenge alianza kupiga soka ya Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2018 baada ya kusajiliwa na mabingwa wa 2009, Sofapaka. Ni miongoni mwa wachezaji 12 ambao walitemwa na Wazito FC mwanzoni mwa wiki hii baada ya kikosi hicho kukiri kwamba hazina yake ya fedha imetikiswa pakubwa na janga la corona.

“Nimekuwa Kenya kwa kipindi cha miaka miwili sasa na azma yangu ni kuondoka humu nchini nikiwa nimejinyakulia ubingwa wa kivumbi cha KPL au taji la mfungaji bora wa ligi hiyo,” akatanguliza.

“Baada ya kuvunja ndoa na Wazito, nina nia ya kutafuta hifadhi kwingineko kwa kipindi cha miaka miwili zaidi kabla ya kurejea DR Congo au kuyoyomea Uswidi ambako wakala wangu anataka sana nielekee,” akasema Kirenge.

Kwa mujibu wa Kirenge, kusalia kwake katika soka ya KPL kutampa jukwaa mwafaka la kujikuza zaidi kitaaluma kadri anavyolenga kupata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya DR Congo almaarufu ‘The Leopards’.

Kirenge aliwajibishwa mara mwisho ndani ya jezi ya timu ya taifa mnamo 2014 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi.