• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Kirui, Kiplagat kuongoza timu ya Kenya kwa Riadha za Dunia

Kirui, Kiplagat kuongoza timu ya Kenya kwa Riadha za Dunia

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imetaja kikosi cha wanariadha tisa wakiwemo mabingwa wa dunia mwaka 2017 Geoffrey Kirui na 2011 na 2013 Edna Kiplagat, kuiwakilisha katika mbio za kilomita 42 kwenye Riadha za Dunia zitakazoandaliwa kutoka Septemba 28 hadi Oktoba 6, 2019, jijini Doha nchini Qatar.

Mbali na Kirui aliyekuwa mshindi wa Boston Marathon mwaka wa 2017, Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), pia limejumuisha katika kikosi cha wanaume Amos Kipruto, ambaye alimaliza Berlin Marathon katika nafasi ya pili mwaka 2018.

Pia mshindi wa Milan City Marathon mwaka 2016, Ernest Ng’eno, bingwa wa Toronto Waterfront Marathon mwaka 2014, Laban Korir na mfalme wa Paris Marathon mwaka 2017 na 2018, Paul Lonyangata, ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu jijini Paris mnamo April 14, 2019.

Naye Kiplagat, ambaye atasherehekea kutimiza umri wa miaka 40 atakapotimka jijini Doha mnamo Septemba 27, atakuwa akishiriki marathon katika Riadha za Dunia kwa mara ya tano mfululizo.

Alishinda nishani ya fedha mwaka 2017 na kumaliza katika nafasi ya tano mwaka 2015.

Atashirikiana na mshindi wa Paris Marathon mwaka 2016, Visiline Jepkesho, ambaye alimaliza Riadha za Dunia katika nafasi ya 20 mwaka 2015.

Wengine ni bingwa wa Sanyo Half Marathon mwaka 2018, Sally Chepyego na malkia wa Dubai Marathon, Ruth Chepng’etich.

Kenya ilipewa nafasi tano katika marathon ya wanaume kwa sababu ilitwaa taji katika makala yaliyopita.

Akizungumzia kikosi cha Kenya, Naibu Rais wa AK, Paul Mutwii alisema, “Ni kikosi kizuri ambacho naamini kila mmoja wao anao uwezo wa kuibuka mshindi kwa sababu wote wanaorodheshwa katika nafasi 20 za kwanza katika viwango bora vya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).”

Kuanza mazoezi

Mutwii alitangaza kwamba kikosi hicho ambacho kitanolewa na makocha Joseph Cheromei na Richard Kimetto, kitaanza mazoezi katika eneo la Kaptagat mapema Julai.

“Mabingwa wa London Marathon mwaka 2019 Eliud Kipchoge na Brigid Kosgei na wa 2018, Vivian Cheruiyot na mshikilizi wa rekodi ya marathon ya wanawake, Mary Keitany, hawangeweza kushirikishwa kikosini kwa sababu wana kandarasi na waandalizi wa mbio kadhaa kubwa duniani mwaka huu,” alieleza.

Aliongeza, “Hawawezi kuvunja kandarasi hizo kwa sababu watapokea adhabu kali wakifanya hivyo.”

Wakati huo huo, alifichua kwamba Kenya mara nyingi huwa na timu ya jumla ya washiriki 60 katika Riadha za Dunia.

  • Tags

You can share this post!

VIDUBWASHA: Simu ya kwanza kutumia masafa ya 5G

TNA wamkana mwasisi Moses Kuria

adminleo