Kisii RFC na Blak Blad zapigwa marufuku
Na CHRIS ADUNGO
KAMATI Huru ya Nidhamu ya Shirikisho Raga la Kenya (KRU) imepiga marufuku klabu za Kisii RFC na Blak Blad kutumia viwanja vyao vya nyumbani katika kampeni za raga ya humu nchini msimu ujao.
Hii ni baada ya vikosi hivyo kupatikana na hatia ya kushindwa kudhibiti mienendo ya wachezaji na mashabiki wao wakati wa mojawapo wa mechi kabla ya shughuli za michezo kusimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona.
Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ndiyo iliyoadhibiwa vikali zaidi kwa kupigwa marufuku ya mechi saba na kwa sasa itahitajika kuchezea zilizokuwa ziwe mechi zao za nyumbani kwingineko.
Adhabu ya awali ya marufuku ya mechi sita kwa kikosi cha Kisii RFC ilipunguzwa hadi michuano mitano baada ya vinara wa klabu hiyo kuungama makosa.
Vikosi hivyo viwili vilishtakiwa kwa kosa la kupuuza usalama baada ya mashabiki wao kujitosa uwanjani kulalamikia utata wa maamuzi ya refa na hivyo kujeruhi baadhi ya wachezaji, mashabiki wenzao na maafisa wa mechi wakati wa tukio hilo.
Matukio hayo yalikuwa kinyume na Kifungu cha Sheria Nambari 20.4 (a) cha KRU kinachoharamisha ghasia au vitisho dhidi ya mtu yeyote ndani ya uwanja wakati mechi inapoendelea.
Kwa mujibu wa mashtaka, klabu husika zilikosa kuhakikisha kwamba mechi zao zinasakatwa katika mazingira bora na mashabiki hawakudhihirisha sifa za uanaspoti mwema.
Kamati ya Nidhamu (ICJ) ilikariri kwamba maafisa wa mchuano hawastahili kuachiwa majukumu ya kutekeleza kanuni zote za mchezo jinsi inavyohitajiwa na Kifungu cha Sheria Nambari 1.1 cha Shirikisho la Raga Duniani.
Mashtaka dhidi ya Blak Blad yalihusiana na mechi iliyokosa kukamilika walipokutana na Kabras RFC mnamo Februari 29, 2020. Mechi hiyo ilisimamishwa na kocha David Ng’etich kunako dakika ya 44. Kwa upande wao, mashtaka dhidi ya Kisii RFC yalihusiana na mechi iliyowakutanisha na Eldoret RFC uwanjani Gusii mnamo Februari 29 vilevile.
Blak Blad ambao awali walikuwa wamepigwa marufuku ya mechi sita katika msimu ujao wa 2020-21 wa kosa jingine la utovu wa nidhamu, waliongezewa adhabu ya mchuano mmoja zaidi kwa hatia ya kutoa maelezo ya kupotosha kuhusiana na rekodi yao ya awali ya nidhamu.