• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Kiungo chipukizi anayelenga kusakata soka Stamford Bridge

Kiungo chipukizi anayelenga kusakata soka Stamford Bridge

NA SAMMY WAWERU

Mtaa wa Githurai ulioko kiungani mwa jiji la Nairobi ni wenye shughuli ainati, kuanzia biashara, shughuli za usafiri na uchukuzi.

Ni mojawapo ya mitaa ambayo ina idadi kubwa ya watu Nairobi na Kiambu, kwa kuwa mtaa huo unapatikana katika kaunti hizo mbili.

Katika mtaa huo huo tunakutana na mvulana Mohamad Said, ambaye ni mwanasoka ukipenda mwanakandanda chipukizi.

Ni mzaliwa wa eneo hilo na mwakani anatarajia kujiunga na kidato cha kwanza. Said alifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane, KCPE mwaka huu, 2019.

Kinyume na vijana wengi wa rika lake hususan wa mijini ambao wakati wao wa ziada na likizo huwa katika vituo vya kompyuta maarufu kama Play Station (PS) kucheza gemu zisizo na manufaa yoyote, muda wake mwingi anautumia kufanya mazoezi ya kabumbu.

Kwa muda ambao amekuwa katika shule ya msingi, Said amekuwa akitumia muda wake wa ziada kunoa kipaji chake katika soka.

Kulingana na simulizi yake, alitambua ana kipaji cha kusakata ngozi iliyoambwa akiwa chini ya umri wa miaka minane. “Nilianza kufuatilia soka nikiwa mchanga kiumri na nimekuwa nikiipalilia talanta yangu,” aelezea Said ambaye ana miaka 13.

Shule ya msingi, mvulana huyo alikuwa akisomea Githurai Primary iliyoko eneo la Githurai 44. Aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba amekuwa mmoja waliowakilisha shule hiyo katika kabumbu, hasa michezo inapoandaliwa.

Peter Nzuki, mchezaji wa Tusker FC ni mmoja wa wanaompa motisha Mohamad Siad na chipukizi wenzake. Picha / SAMMY WAWERU

“Nimekuwa katika timu ya soka ya Githurai Primary. Nimeshiriki mechi kadha baina ya timu mbalimbali za shule eneo la Githurai, michuano inapoandaliwa,” asema.

Ni kiungo wa kati, ambaye jukumu lake kuu limekuwa kudifendi timu anayowakilisha. Staa Said pia anasema husakata ngoma katika wingi ya midifilda wa kati. “Aghalabu hutanikosa nimewekwa nambari ya nne,” adokeza chipukizi huyo.

Katika muundo wa mchezo wa kandanda, madifenda ni kati ya nambari 2 hadi 6. Aidha, nambari 4 na 5 ni viungo madifenda wa kati.

Nao 3/2 wanajukumika wing’i ya kushoto na kulia, pande zote uwanjani ili kuzuia wapinzani na mikwaju yao. Nambari 4 au 6 ni difenda midifilda.

Kulingana na Fredrick Ochieng, ambaye ni kocha wa Mohamad Said, amekuwa akipalilia staa huyo katika wing’i nambari 4 tangu akiwa mdogo, alipoonesha mapenzi yake katika kandanda.

“Nilipompokea na kutangamana naye kwa muda, niligundua ana uwezo kuwa defenda kiungo nambari nne. Pia anaweza kucheza nambari sita,” aeleza Bw Ochieng, akisifia juhudi za kipaji huyo.

Kocha wa chipukizi huyo Bw Fredrick Ochieng. Anasema ni kiungo gwiji wa kati. Picha/ Sammy Waweru

Mdau huyo pia anafichua kwamba ana vipaji chungu nzima anaonoa chini ya timu ya All Stars Githurai na Githurai United. Kocha Ochieng amegawanya mafunzo ya vipaji kwa mujibu wa umri; walio chini ya umri wa miaka 10, miaka 11 – 12, wa 13 – 16 na zaidi ya 18.

Ili kuendelea kupalilia talanta yake, Mohamad Said ana matamanio kujiunga na shule ya upili inayotilia mkazo masuala ya soka, akitaja mojawapo kama Kakamega High ambayo ni tajika katika kabumbu nchini.

Wakati wa mahojiano alisema ndoto zake ni kusakatia ngoma timu ya kitaifa hapa nchini Harambee Stars na kilabu ya Gor Mahia. “Hata ingawa Michael Olunga ni straika, ninavutiwa na anavyocheza,” Said akafichua mwanasoka tajika anayemuiga.

Bw Olunga ni staa Mkenya anayechezea kilabu ya Kashiwa Reysol, nchini Japan. Pia amewahi kuchezea Harambee Stars, Tusker FC, Gor Mahia na Thika United.

Katika timu zinazoshiriki michuano ya EPL, Said anasema anashabikia Chelsea, akijaribu kuiga nyayo za midifilda wake Christian Pulisic. “Nina matumaini ipo siku nitachezea Chelsea,” asema.

Wakati wa mazoezi, hutakosa kumpata Said akitangamana na mastaa waliobobea katika vilabu mbalimbali. Peter Nzuki wa Tusker FC ni mmoja wa masahibu wake.

“Chipukizi kama hawa tunajaribu kuwaleta karibu nasi ili wafuatilie tunavyofanya mazoezi na kushiriki mechi, ikiwa ni pamoja na kuwapa mashauri,” aeleza Bw Nzuki.

Ili kuafikia ndoto zake na kuchezea timu anazotamani siku za usoni, Patrick Ogwayo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya soka anahimiza haja ya staa huyo kupewa nafasi ya kipekee kutangamana na timu anazomezea mate ikiwa ni pamoja na zile tajika.

Bw Ogwayo pia anasema fursa ya kukutana ana kwa ana na wachezaji gwiji kutamuwezesha kufunguka kimawazo.

“Wachezaji chipukizi wakipata mwanya wa kutangamana na timu tajika na wachezaji wake watapata motisha na mashauri kwa kina namna ya kufua dafu katika ulingo wa soka. Kila mchezaji ana hadithi yake alipovyofikia alipo sasa, hivyo basi watawafaa zaidi,” afafanua.

Hata hivyo, ukosefu wa fedha ni baadhi ya changamoto zinakumba wengi wa wachezaji wanaoinuka, suala ambalo linatishia kuzima ari yao. Kulingana na Ogwayo, vipaji wengi wangekuwa na uga bora, sare na hata magwanda wangefanya makuu.

“Wengi wao hawana uwezo kuimarisha talanta zao na namna ya kufika katika uga kushuhudia mechi za kitaifa. Wanapaswa kupigwa jeki,” ashauri mdau huyo, akitaja asasi husika kama wizara ya michezo na viongozi kuwa katika mstari wa mbele.

Kauli ya mtaalamu huyo hasa kuhusu ufadhili na uga inasisitizwa na Kocha Fredrick Ochieng, akieleza kuwa hiyo ndizo changamoto kuu zinazowazingira.

Isitoshe, analalamika kwamba juhudi zake na makocha wenza na wakufunzi kufikia wadau husika zimeambulia patupu kwani hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.

“Hebu mwenyewe tazama uwanja tunaochezea, ni vumbi tupu,” akaambia Taifa Leo Dijitali.

 

You can share this post!

‘Nidhamu ilitusaidia kuwika KCSE’

Watahiniwa walemavu waongezeka, wang’aa

adminleo