Michezo

Kiungo Gareth Barry astaafu soka akiwa na umri wa miaka 39

August 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

ALIYEKUWA mwanasoka wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Barry, ameangika rasmi daluga zake kwenye ulingo wa kabumbu akiwa na umri wa miaka 39.

Barry anastaafu soka baada ya kusakata jumla ya michuano 653 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mwanadimba huyo alifunga jumla ya mabao 53 na kuchangia mengine 64 katika kipindi cha usogora wake kwenye kivumbi cha EPL.

Akiwa miongoni mwa viungo waliochukuliwa kuwa bora zaidi enzi yake, Barry aliwajibishwa na timu ya taifa ya Uingereza mara 53 kati ya 2000 na 2012.

Alianza kupiga soka ya kitaalamu akivalia jezi za Aston Villa kabla ya kujiunga na Manchester City kwa kima cha Sh1.7 bilioni mnamo 2012.

Akiwa Man-City, aliwajibishwa mara 175 katika kipindi cha misimu minne iliyomshuhudia akipachika wavuni mabao manane na kuchangia mengine 18.

Aidha, aliwasaidia Man-City kunyanyua taji la EPL na ubingwa wa Kombe la FA.

Baada ya kuridhisha vinara wa Everton wakati akichezea kikosi hicho kwa mkopo, nyota huyo alipokezwa mkataba wa kudumu ugani Goodison Park mnamo 2014.

Baada ya kuchezea Everton kwa miaka mitatu, Barry alihamia West Bromwich Albion mnamo 2017.