Michezo

KIVUMBI CARABAO: Patashika Carabao Cup iking'oa nanga

September 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

MANCHESTER City wataanza kampeni za kutetea ubingwa wa Kombe la Carabao almaarufu EFL au League Cup hii leo Jumanne dhidi ya Preston North End uwanjani Deepdale, Uingereza.

Katika mechi nyinginezo za leo Jumanne, Arsenal waliowabwaga Aston Villa 3-2 wikendi iliyopita watakuwa wenyeji wa Nottingham Forest uwanjani Emirates huku Tottenham Hotspur ikiwaendea wanyonge Colchester.

Southampton watapimana ubabe na Portsmouth ugenini, Sheffield Wednesday waialike Everton nao Watford wawe wenyeji wa Swansea City ugani Vicarage Road.

Man-City watashuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo bila ya huduma za mabeki Aymeric Laporte na John Stones wanaouguza majeraha ya goti na paja mtawalia. Isitoshe, kikosi hicho cha mkufunzi Pep Guardiola kitakosa pia maarifa ya kiungo Leroy Sane aliyehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Bayern Munich mwishoni mwa msimu uliopita.

Kwa upande wa Preston, nahodha na beki tegemeo Tom Clarke atakuwa nje ya kikosi hicho kitakachokosa pia huduma za mvamizi matata Louis Moult. Wawili hao wanauguza majeraha ya magoti.

Mchuano huo utaamuliwa na refa mzoefu Lee Mason ambaye atasaidiana na Marc Perry, Nick Hopton na Tony Harrington.

Chini ya Guardiola, Man-City wanatazamiwa kuendeleza ubabe wao katika kivumbi hicho hasa ikizingatiwa ukubwa wa hamasa iliyowashuhudia wakiwapepeta Watford 8-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mabao matano yaliyofungwa na Man-City chini ya dakika 18 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza dhidi ya Watford yaliwafanya kikosi cha kwanza kuwahi kufunga magoli mengi zaidi ya haraka katika kivumbi cha EPL.

Ilikuwa ni mechi ya 12 kwa Watford kupoteza dhidi ya Man-City ambao wameapa kunyanyua ufalme wa taji la EPL kwa mara ya tatu mfululizo msimu huu, kutetea kwa mafanikio taji la Carabao Cup, kutia kapuni Kombe la FA na kupiga hatua kubwa zaidi katika kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mabao yaliyofungwa na Man-City dhidi ya Watford ndiyo idadi kubwa zaidi ya magoli kuwahi kurekodiwa katika historia ya soka ya EPL. Isitoshe, kichapo hicho ndicho kinono zaidi kuwahi kupokelewa na Watford waliowahi pia kupepetwa 8-1 na Aberdare Athletic na 8-1 na Crystal Palace mnamo Januari 1926 na Septemba 1959 mtawalia.

Ushindi wa Man-City katika mechi hiyo uliwapa rekodi ya kuwa kikosi cha kwanza baada ya Chelsea kuwahi kufunga timu moja ya EPL zaidi ya mabao sita chini ya kipindi cha misimu miwili. Chelsea waliwahi kusajili ushindi wa zaidi ya mabao sita katika michuano miwili ya ligi dhidi ya Wigan Athletic mnamo 2010.

Bao la David Silva lilikuwa la haraka zaidi kuwahi kupachikwa wavuni katika kivumbi cha EPL hadi kufikia sasa msimu huu. Ni mchuano uliompa kiungo De Bruyne jukwaa la kuweka historia ya kuwa mchezaji ambaye kwa sasa amechangia idadi kubwa zaidi ya mabao (52) katika EPL.

Aguero kwa sasa ndiye mchezaji wa kwanza baada ya Romelu Lukaku wa Inter Milan kuwahi kufunga bao katika jumla ya mechi saba mfululizo za EPL. Lukaku aliyeagana na Manchester United mwishoni mwa msimu jana, aliiweka rekodi hiyo mnamo Disemba 2015 akivalia jezi za kikosi cha Everton chini ya mkufunzi David Moyes.

Baada ya kuvaana na Preston, Man-City watakuwa wageni wa Everton ugani Goodison Park nao Watford waalikwe na Wolves katika uwanja wa Molineux.

Preston watajibwaga ugani kwa minajili ya mechi ya leo wakijivunia motisha tele baada ya kuwabamiza Birmingham City 1-0 ugenini katika mchuano uliopita wa Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza.

Itakuwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 10 kwa Preston na Man-City kukutana. Vikosi hivyo vilionana kwa mara ya mwisho mnamo Februari 2007 katika raundi ya tano ya Kombe la FA uwanjani Deepdale.

Katika mchuano huo, Man-City waliibuka na ushindi wa 3-1. Mabao ya Man-City wakati huo yalifumwa wavuni kupitia kwa Michael Ball na Stephen Ireland aliyejifunga baada ya David Nugent kuwapa wenyeji uongozi wa mapema katika kipindi cha kwanza.

Ratiba ya Carabao Cup (Leo Jumanne)

Arsenal na Nottingham Forest

Colchester Utd na Tottenham

Crawley Town na Stoke City

Luton Town na Leicester City

Portsmouth na Southampton

Preston North End na Man-City

Sheffield Wed na Everton

Watford na Swansea City

(Jumatano):

Brighton na Aston Villa

Burton Albion na Bournemouth

Chelsea na Grimsby Town

Milton Keynes na Liverpool

Oxford Utd na West Ham Utd

Sheffield Utd na Sunderland

Wolves na Reading

Man-Utd na Rochdale