Kivumbi chatarajiwa Thika Queens na Gaspo Women wakivaana
Na JOHN KIMWERE
KIVUMBI kikali kinanukia wikendi hii baina ya Thika Queens na Gaspo Womens katika Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL), nayo Vihiga Queens inapigiwa chapuo kuvuna alama sita muhimu baada ya kucheza mechi mbili.
Mabingwa watetezi, Vihiga Queens ya kocha, Alex Alumirah Jumamosi hii itakuwa ugenini kuvaana na Kisumu Allstarlets uwanjani Moi Stadium mjini Kisumu, kisha Jumapili itasafiri mjini Eldoret kugarazana na wenyeji wao Eldoret Falcons.
”Hatutakuwa na la ziada mbali tumepania kujibiidisha kadiri ya uweza wetu kusaka ushindi wa alama zote muhimu,” kocha wa Vihiga alisema.
Nayo Thika Queens ya kocha, Benta Achieng itakuwa katika ardhi ya nyumbani kukaribisha Gaspo kwenye mechi inayotazamiwa kuzua msisimko wa kufa mtu.
Bila shaka tunatarajia mtihani mgumu mele ya wageni wetu,” alisema ofisa mkuu wa Thika, Fredrick Chege na kuongeza kuwa watajitahidi kutafuta ushindi wa alama zote muhimu.
Kwenye mchezo wa mkumbo wa kwanza, Gaspo ilitwaa ufanisi wa magoli 4-3.
Kwenye mfululizo wa kipute hicho, Mathare United Women (MUW FC) itamenyana na Zetech Sparks (Soccer Queen) uwanjani Stima Club nayo Kayole Starlets itakwaruzana na Kibera Girls Soccer Academy (KGSA).
Mathare itaingia mzigoni ikijivunia kubeba ufanisi wa magoli 3-1 dhidi ya Oserian Ladies licha ya kudondosha patashika moja mbele ya Gaspo wiki iliyopita.
Kwenye msimamo wa kinyang’anyiro hicho, Gaspo Womens ingali kifua mbele kwa alama 63 baada ya kucheza mechi 23.
Nayo Vihiga Queens inakamata mbili bora kwa kufikisha pointi 58, sawa na Trans Nzoia Falcons kutokana na mechi 21 na 23 mtawalia. Malkia wa zamani, Thika Queens inashikilia nne bora kwa alama 56, 16 mbele ya Kisumu All Starlets.