• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kivumbi Gulf African Bank ikivaana na ECO Bank

Kivumbi Gulf African Bank ikivaana na ECO Bank

Na JOHN KIMWERE

USHINDANI mkali unatazamiwa kushuhudiwa kwenye mechi za robo fainali kuwania ubingwa wa mashindano ya Mashirika ya Kifedha nchini (Interbanks) makala ya mwaka huu yanayoendelea katika Uwanja wa KSMS, Nairobi.

Gulf African Bank (GAB) ya kocha, Abdul Aziz itavaana na ECO Bank uwanjani Stima Club, Thika Road Nairobi.

GAB ilijikatia tiketi ya mchezo huo ilipozaba Bank of Africa (BOA) magoli 3-1 na kutinga mbili bora Kundi B, kwa alama kumi ikifuata BOA iliyokusanya pointi 15.

Gulf ilipata ufanisi huo kupitia Bakari Mahora aliyepiga kombora mbili safi huku Hamza Ahmed akiitingia goli moja. Kwenye mechi za awali kundi hilo, GAB iliilaza Agricultural Finance Corporation (AFC) mabao 2-0, ilikomoa Chuo Kikuu cha JKUAT bao 1-0 kisha ilitoka nguvu sawa magoli 3-3 dhidi ya Stanbic Bank.

”Nashukuru vijana wangu kwa kusonga mbele lakini nawaambia lazima wajitahidi kukabili wapinzani wetu kwenye robo fainali,” alisema kocha huyo wa GAB na kuongeza kuwa wanafahamu haitakuwa rahisi pia hawawezi kudharau wapinzani wao.

ECO Bank ilimaliza kileleni mwa Kundi D kwa alama nane sawa na Central Bank of Kenya (CBK) tofauti ikiwa idadi ya magoli. Kwenye mechi za mwisho Kundi hilo, CBK ililaza BBK goli 1-0 huku I &M ilkichapwa magoli 3-1 na ECO Bank.

Nao mabingwa wa Kundi A, Equity Bank waliovuna alama 13, mbili mbele ya KCB itashuka katika Uwanja wa Barclays Bank kumenyana na National Bank of Kenya (NBK) ya kocha, Wilfred Osaso iliyozoa pointi 14 na kumaliza ya pili Kundi C.

Katika robo fainali ya tatu, Uwanjani Survey, Consolidated Bank itaingia mzigoni kucheza na KCB huku wachezaji wa BOA wakikutanishwa na CBK katika Uwanja wa KSMS. Consolidated Bank ilinasa tiketi ya kushiriki robo fainali ilipoandikisha alama 14 ikiwa kifua mbele Kundi C.

Kwenye matokeo mengine, StanChart ilituzwa alama tatu bila jasho baada ya wapinzani wao AFC kuingia mitini. Wachezaji wa Paramount walipiga Kenya Bankers Sacco mabao 3-1, NIC ikiagana sare ya bao 1-1 na NBK nayo Consolidated Bank ilibeba ufanisi wa mabao 3-0 dhidi ya Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN).

  • Tags

You can share this post!

Polisi motoni katika kesi ya kifo cha Samuel Wanjiru

SHINA LA UHAI: Tatizo la maumbile lifanyalo matiti kuwa...

adminleo